Wednesday, August 10, 2016

WATUMISHI IDARA YA AFYA MBINGA WAITAKA SERIKALI KUWALIPA MADAI YAO


Sixtus Mapunda, Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini akisisitiza jambo katika kikao alichoketi jana wakati akizungumza na watumishi wa idara ya afya katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

WATUMISHI wa idara ya afya hospitali ya Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wameutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuwalipa madai yao ya aina mbalimbali ili waweze kutatua matatizo yao yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Watumishi hao wakichangia hoja mbalimbali.
Madai hayo walifafanua kuwa ni malimbikizo ya fedha za likizo, matibabu na safari ambapo hawajalipwa kwa muda mrefu sasa na hawajui hatima yake kwa kile walichoeleza kuwa wamekuwa wakifuatilia mara kwa mara, kwa uongozi husika na hakuna dalili zinazoonesha kuzaa matunda.

Hayo yalisemwa jana na watumishi hao walipokuwa wakizungumza na Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda ambaye aliwatembelea hospitalini hapo kwa lengo la kusikiliza na kupokea kero zao za aina mbalimbali ili ziweze kufanyiwa kazi.

Raymond Ngatunga ambaye naye ni muuguzi wa hospitali hiyo alieleza kuwa yeye na watumishi wenzake wamekuwa wakidai madai hayo kwa muda mrefu, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuona umuhimu wa kutekeleza jambo hilo mapema ili waweze kuondokana na mazingira magumu katika kusukuma mbele maisha yao.


Kadhalika baadhi yao walilalamikia suala la kutothibitishwa kazini, licha ya kwamba wamefanya kazi hospitalini hapo kwa muda mrefu.

Akitolea majibu juu ya madai hayo kwa niaba ya Mbunge huyo, Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Elisha Robert alikiri juu ya watumishi hao kudai madai hayo na wengine kutothibitishwa kazini ambapo halmashauri inafanya jitihada ya kumaliza kero hiyo ikiwemo kulipa madeni hayo.

“Mheshimiwa Mbunge, hata hospitali pia imekuwa ikidaiwa bili za maji na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira bado hayajalipwa kwa muda mrefu, tunaomba wawe wavumilivu tutawalipa kulingana na kiasi cha fedha tutakachoanza kupokea kutoka serikalini”, alisema Dkt. Robert.

Kwa upande wake Mbunge, Mapunda alisisitiza kwa kuutaka uongozi husika katika halmashauri ya mji wa Mbinga kuhakikisha kwamba madai ya watumishi hao yanalipwa kwa wakati ikiwemo pia suala la kuwathibitisha kazini, ili waweze kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na sio kuwa na manung’uniko yasiyokuwa na kikomo.

“Hawa watu wanataka haki zao, mtu anayedai deni lake ni lazima ulipe hivyo nasisitiza kwa mamlaka husika kulifanyia kazi tatizo hili haraka, ili tuweze kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima”, alisema Mapunda.

Pamoja na mambo mengine Mbunge huyo aliwataka watumishi wa idara ya afya katika hospitali hiyo kujenga ushirikiano, kuwa wazi wakati wote katika utendaji wao wa kazi na kuacha majungu.

No comments: