Sunday, August 28, 2016

MTOTO AJINYONGA CHUMBANI KWAKE BAADA YA KUCHOSHWA NA KAULI MBAYA ZA MAMA YAKE MZAZI

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

MTOTO Zawadi Hassan (14) mkazi  wa kitongoji cha Majengo kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, amejinyonga kwa kutumia chandarua chake wakati akiwa chumbani kwake baada ya kuchoshwa  na kauli zisizokuwa na staha kutoka kwa  mama yake mzazi ambaye hakufahamika jina lake mara moja.

Tukio hilo limetokea  mwishoni mwa wiki ambapo mwili wa marehemu huyo ulikutwa chumbani kwake asubuhi siku ya Ijumaa, baada ya mama huyo kumtaka aamke na ndipo jitihada za kumwita mlangoni ziligonga mwamba ambapo alipochukua jukumu la kufungua mlango, aliukuta mwili wa mwanae ukiwa juu unaning’inia.

Mtendaji wa kata ya Mkongo, Whiclif Mtinda alikwenda katika eneo la tukio na kuthibitisha kifo cha kijana huyo kilichosababishwa na kujinyonga kwa kutumia chandarua kutokana na  kauli za kuudhi kutoka  kwa mama yake  mzazi.


Kwa mujibu wa  Mtinda alieleza kuwa kabla ya kwenda kulala marehemu alikuwa anadai hela yake kutoka kwa mama yake ambazo alimpatia mama huyo amwekee na alipozihitaji, mama huyo alikuwa akimtolea maneno yasiyokuwa mazuri na ndipo mtoto huyo aliamua kuchukua maamuzi hayo magumu.

Malumbano ya mama na mwanae yaliendelea na kumtaka mwanae  aondoke na aende kuishi na baba yake mzazi, kwa kuwa baba ya mtoto huyo na mama yake waliachana miaka mingi iliyopita.

“Kitendo cha mama huyu kumweleza mtoto wake aende akaishi  kwa baba yake  na kumnyima fedha zake alizoziweka kwake, ndipo alikasirika na kuamua kujinyonga”, alisema Mtinda.


Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kujinyonga kwa mtoto huyo ambapo marehemu amezikwa katika kijiji cha Mkongo na kwamba Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

No comments: