Tuesday, August 9, 2016

WAPEWA MAFUNZO YA KUZUIA MAAMBUKIZI MAPYA YA VIRUSI VYA UKIMWI

Mji wa Songea.


Na Muhidin Amri,       
Songea.

WATU waliopo katika makundi maalum katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamepatiwa mafunzo ya kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi ili waweze kuepukana na maambukizi hayo.

Zaidi ya watu 80 ndio waliopewa mafunzo hayo ya siku mbili mjini hapa, ambapo makundi hayo yalipata elimu juu ya ukweli kuhusu Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI, matumizi sahihi ya kondomu ikiwemo za kike na kiume pamoja na madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya.

Mratibu wa Ukimwi na tiba Manispaa ya Songea, Dkt. Felista Kibena alisema makundi ambayo yamenufaika na mafunzo hayo ni watu wanaofanya biashara ya ngono, wanaofanya ngono  ya jinsia moja na watu wanaojidunga sindano pamoja na watumiaji wa unga na madawa hayo ya kulevya.


Kibena alisema kuwa idara yake imeamua kutoa elimu hiyo juu ya ukweli kuhusu magonjwa hayo, baada ya utafiti kubaini kwamba makundi hayo sasa yanaongoza kwa kiwango kikubwa cha maambukizi.

Alifafanua kuwa njia ambazo zinaongoza kwa maambukizi mapya ya ukimwi ni  kupitia ngono ya kawaida isiyo salama na mtu aliyehatarini au aliyeambukizwa kutoka kwa mama aliyeambukizwa kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua au kunyonyesha.

Njia nyingine ni Kupitia sindano zilizoambukizwa kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya sindano, kupitia njia ya ulawiti kwa mwanamume kwa mwanamume kwa mwanamume kwa mwanamke na kupitia uchangiaji wa vifaa vya kuchanjia au kudungia na wakati wa tohara.

“Tumefanikiwa kutoa elimu ya kutosha kuzuia maambukizi ya virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, hali hiyo imesababisha watoto waliozaliwa na VVU wamekuwa na afya nzuri baada ya kuwaanzishia dawa za kurefusha maisha (ARVS) na hivi sasa wengi wao wanasoma sekondari na vyuo vikuu’’, alisema.

Mratibu huyo aliongeza kuwa utafiti umebaini kwamba matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 45 bado ni tatizo kubwa katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.

Kwa upande wake, Ofisa habari wa Manispaa hiyo Albano Midello alisema kuwa takwimu zilizopo mjini hapa zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 kulikuwa na waathirika wa dawa za kulevya 145 kati ya hao wanaume 138 na wanawake walikuwa saba.

Alieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Mei mwaka huu Manispaa hiyo ina jumla ya waathirika wa dawa hizo 97 kati yao, wanawake wawili na wanaume 95 ambapo waathirika wote hawa wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 45.

No comments: