Monday, August 22, 2016

ASHIKILIWA NA POLISI KWA KUMILIKI SILAHA KINYUME CHA SHERIA

Na Kassian Nyandindi,          
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Filbert Moyo (40) mkazi wa kijiji cha Tingi wilaya ya Nyasa mkoani humo kwa kukutwa na silaha mbili aina ya Gobole ambazo zimetengenezwa kienyeji.

Aidha Jeshi hilo linamsaka mtu mwingine ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Malumba wilayani Tunduru mkoani hapa kwa kukutwa na silaha aina ya SMG ikiwa na risasi 23.

Zubery Mwombeji, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Kaimu kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Dismas Kisusi alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea Agosti 13 mwaka huu majira ya saa 11:30 asubuhi huko katika wilaya ya Nyasa ambako askari Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na silaha hizo.

Kisusi alisema kuwa silaha hizo alikuwa amezihifadhi kwenye mfuko katika eneo la Ngurumashamba kwenye hifadhi ya wanyama ya Liparamba iliyopo wilayani humo.


Alifafanua kuwa Polisi walipata taarifa kwamba Moyo anamiliki silaha kinyume na sheria za nchi ndipo walipokwenda huko kumfuatilia, walifanikiwa kumkamata na kwamba upelelezi juu ya tukio hilo bado unaendelea kufanywa utakapokamilika atafikishwa Mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Kadhalika alilitaja tukio jingine kuwa Agosti 14 mwaka huu majira ya asubuhi huko katika kitongoji cha Malando kijiji cha Malumba tarafa ya Nalasi  wilayani Tunduru askari Polisi wakiwa kwenye doria, walifanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja na baadaye aliwakimbia na kuitupa silaha moja aina ya SMG yenye namba za usajili 1952 KMI.

Alieleza kuwa katika silaha hiyo kulikuwa na risasi 23 na kwamba tukio hilo lilitokea karibu na ofisi ya kijiji hicho na jitihada ya kumsaka mtuhumiwa huyo zinaendelea.


Hata hivyo Kisusi alitoa rai kwa mtu yeyote anayetumia au kumiliki silaha kinyume na taratibu za nchi ni vyema akaona umuhimu wa kusalimisha silaha yake mara moja, ili zifanyiwe uchunguzi na wamiliki halali wazisajiri mapema kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

No comments: