Wednesday, August 31, 2016

TAHARUKI YAIBUKA MADENI YA MIKOPO ELIMU YA JUU NAMTUMBO

Na Mwandishi wetu,         
Namtumbo.

KUFUATIA kutolewa  kwa orodha  ya  majina ya wadaiwa sugu ya mkopo wa elimu ya juu, kumeibuka taharuki kwa baadhi ya watumishi wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kuingizwa kwenye orodha  ya wadaiwa hao, licha ya kutosoma elimu ya juu na kutohusika kuomba mkopo huo.

Kwa mujibu wa Ofisa habari wa wilaya hiyo, Yeremias Ngerangera amethibitisha kupokea malalamiko kutoka kwa walimu sita wa shule za msingi wilayani humo ambao wanadai kuwa hawajasoma elimu hiyo ya juu na hawakuomba fedha hizo kutoka bodi ya mikopo.

Aidha Ngerangera aliwataja walimu waliowasilisha malalamiko yao wilayani humo kuwa ni  mwalimu Thomas Komba ambaye anadaiwa shilingi 3,444,030, Joseph Chengura anayedaiwa 12,911,370 na mwalimu Michael Haulle anayedaiwa shilingi 2,733,099 na bodi ya mikopo elimu ya juu.


Vilevile aliwataja wengine kuwa ni mwalimu Michael Jimmy anayedaiwa shilingi 29,125,905 mwalimu Deogratias Haulle anayedaiwa shilingi 16,055,100 na  Marry Haulle anayedaiwa shilingi 2,643,518 ambao wote wanailalamikia bodi hiyo kwa  kuingizwa kwenye orodha ya madeni hayo wakati wao hawajawahi kuomba fedha hizo kwa ajili ya kwenda kusoma.

Ofisa habari huyo wa wilaya ya Namtumbo alifafanua kuwa halmashauri ya wilaya hiyo inaendelea kupokea malalamiko kama hayo ya walimu wote wa shule za msingi na sekondari kwa maandishi, ili yaweze kuwasilishwa kwenye bodi ya mikopo kwa uchunguzi  na kuchukuliwa hatua zaidi.

Walimu hao walikwenda kwa Ofisa habari huyo kuelezea masikitiko yao juu ya kuingizwa kwenye orodha ya madeni  ya wadaiwa sugu, huku wakidai kuwa endapo serikali haitaweza kuchukua hatua dhidi ya wahusika waliofanya ujanja huo wapo tayari kuomba msaada wa kisheria popote pale ili waweze kumaliza tatizo hilo.


Hata hivyo uongozi husika wa halmashauri ya wilaya  ya Namtumbo, umewataka walimu wote kuwasilisha vielelezo vyao mapema wakiwemo na watumishi wengine ambao wanadai kwamba hawakusoma elimu ya juu huku wakati huo wakiwa wameingizwa kwenye orodha ya wadaiwa sugu, ili kuweza kupeleka malalamiko yao kwa bodi ya mikopo kwa uchunguzi wa madai yao.

No comments: