Saturday, August 20, 2016

WATENDAJI MBINGA WATAKIWA KUKUSANYA MAPATO IPASAVYO

Aliyesimama ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gombo Samandito akisisitiza jambo katika kikao cha baraza la Madiwani wilayani humo ambacho kilifanyika hivi karibuni.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

WATENDAJI wa vijiji na kata katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kukusanya mapato ya halmashauri hiyo kwa kuhakikisha kwamba wanadhibiti mianya inayoweza kupoteza mapato hayo, ili fedha zitakazopatikana ziweze kwenda kufanya kazi za maendeleo ya wananchi.

Vilevile wameagizwa kuendelea kuimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato hayo kwa kutumia mfumo wa mashine maalumu za kieletroniki (EFD’S) ili kuweza kudhibiti wizi unaoweza kutokea kwa wale watendaji wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa na mazoea ya kuiibia serikali.

Gombo Samandito ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, alisema hayo juzi alipokuwa akitoa maelekezo mbalimbali ya kikazi kwa watendaji hao katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika mjini hapa.


“Tujitahidi kuziba mianya inayoweza kupoteza mapato ya halmashauri yetu, watendaji wote tunapaswa mtusaidie kusimamia ukusanyaji wa mapato tuimarishe mifumo yetu ya ukusanyaji, ili tuweze kufikia ipasavyo malengo yetu tuliyojiwekea”, alisema Samandito.

Pia alitoa agizo kwa kuwataka wataalamu husika wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kuanza mara moja zoezi la upimaji wa maeneo ya wazi ili kuweza kutenga maeneo ya makazi, uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo.


“Ni vyema ndugu zangu wakati wa upimaji tusisahau kutenga maeneo haya kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wetu, pia kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye”, alisema.
Alisisitiza kwamba jukumu kubwa la viongozi wa serikali ni kuwahudumia wananchi ipasavyo, hivyo kiongozi yeyote katika eneo lake akishindwa kutekeleza majukumu yake aliyopewa maana yake ameshindwa kuwajibika na kwamba yupo tayari kumchukulia hatua kali za kisheria, ikiwemo kumfukuza kazi.

No comments: