Sunday, August 28, 2016

NAMTUMBO KUZALISHA TANI 600 ZA TUMBAKU

Zao la tumbaku.
Na Yeremias Ngerangera,        
Namtumbo.

WAKULIMA wanaozalisha tumbaku katika kata ya Mgombasi wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, katika msimu wa mwaka 2016/2017 wanatarajia kuzalisha tani 600 za zao hilo wilayani humo.

Hayo yalisemwa na diwani wa kata ya Mgombasi wilayani hapa, Mrisho Mbawala mbele ya Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Ally Lugendo wakati wa ziara ya kuhamasisha wakulima hao wazalishe tumbaku kwa wingi kwa kuzingatia mbinu za kilimo bora cha kisasa.

Mbawala alifafanua kuwa wataweza kuzalisha kiasi hicho katika msimu huo kutokana na uliopita, walikuwa wakizalisha tani 60 tu kufuatia wakulima wengi kukata tamaa juu ya uzalishaji huo.

Aidha alieleza kuwa sababu kuu ya ongezeko hilo linatokana na wakulima wengi kuhamasika kulima tumbaku, ambapo katika kipindi cha mwaka 2015/2016 kulikuwa na wakulima 150 na sasa wamefikia wakulima 400.


Pia alitaja sababu ya ongezeko la wakulima hao linatokana na serikali kuwahakikishia itasimamia kikamilifu juu ya malipo ya fedha zao za tumbaku itakayouzwa sokoni, tofauti na hapo awali wakulima walikuwa hawalipwi ipasavyo.

“Katika misimu mitatu iliyopita wakulima walikuwa hawalipwi fedha zao kutokana na vyama vyao vya msingi kuwa na madeni makubwa, kutoka kwa wakopeshaji wa pembejeo za kilimo jambo ambalo liliwafanya waache kuzalisha zao hili”, alisema Mbawala.

Kwa upande wake Ofisa kilimo wa wilaya ya Namtumbo, Lugendo alisema kuwa atahakikisha ofisi yake inasimamia upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima wa tumbaku wilayani humo kwa kuzingatia misingi na taratibu husika ili wasiweze kudhulumiwa na hatimaye kushindwa kuzalisha zao hilo kwa wingi.

Pia aliwahakikishia kwamba, watapata malipo yao mara baada ya mauzo kufanyika ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima wakulima kukosa fedha zao.

Lugendo aliwataka wakulima hao kuwa waaminifu pale wanapokopeshwa pembejeo za kilimo ambapo wanapaswa kulipa kwa wakati, mara baada ya tumbaku yao kuuzwa sokoni.


Kata ya Mgombasi ina jumla ya vyama vya ushirika vitatu vinavyojishughulisha na uzalishaji wa zao hilo ambavyo ni Mgombasi, Nangero na Nambecha ambapo kwa msimu wa mwaka 2015/2016 wakulima walizalisha tani 60 zilizowawezesha  kulipwa shilingi milioni 155,595,000.

No comments: