Sunday, August 21, 2016

CHIKAMBO AWATAKA WANAWAKE RUVUMA KUMPATIA USHIRIKIANO



Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

MBUNGE wa Viti maalum mkoani Ruvuma, Sikudhan Chikambo amezitaka Halmashauri za wilaya mkoani humo kutekeleza jukumu la kupeleka asilimia 10 ya fedha za mapato yake ya ndani katika vikundi vya ujasiriamali, kwa wanawake na vijana.

Aidha amewaagiza madiwani wa mkoa huo, kuhakikisha kwamba suala hilo wanalifuatilia kwa karibu ndani ya halmashauri zao kupitia vikao husika, ili fedha hizo zielekezwe kwa kundi hilo.

Chikambo alitoa agizo hilo juzi, alipokuwa akizungumza na akina mama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Mbinga, katika kikao cha baraza la wanawake kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini hapa.

Mbunge huyo alisema kuwa wanawake wanaweza kujituma kwa kila jambo la kimaendeleo, hivyo wanapaswa wakati wote kutetea haki zao pale wanapoona zinaporwa na watu wasiopenda maendeleo yao.


“Madiwani mliochaguliwa nawataka pia mrudi kwenye kata zenu kutumikia wananchi na sio muda mwingi kuwa mbali, tuache sasa tabia ya kutengeneza majungu na fitina tuunge mkono kauli mbiu ya Rais wetu John Magufuli, ‘Hapa kazi tu’ kwa kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maendeleo ya taifa letu”, alisema Chikambo.

Vilevile aliwataka wanawake kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, ili waweze kujikwamua katika maisha yao ya kila siku na sio muda mwingi kulalamika na kukaa bila kujishughulisha katika kazi mbalimbali.

“Mimi binafsi nina ahidi kufanya kazi na wanawake wote wa mkoa wa Ruvuma naomba nipeni ushirikiano, jukumu hili la ubunge mlilonipatia linahitaji ushirikiano wa dhati, upendo na uaminifu ili tuweze kufikia malengo ya kimaendeleo tuliyojiwekea”, alisisitiza Chikambo.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya UWT wilaya ya Mbinga, Katibu wa umoja huo wilayani humo, Martina Katyale alisema kuwa wanachama wamejiwekea mikakati ya kuimarisha miradi waliyonayo ya kimaendeleo ikiwemo kuongeza upandaji wa miti ya mbao, kwa msimu wa mwaka 2016/2017 ngazi ya kata na matawi.

Hata hivyo Katyale aliongeza kuwa katika kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri kwa wanachama wake, uongozi wa umoja wa wanawake ngazi ya wilaya utafanya ziara ya kuwatembelea wanawake katika kata zote 48 kwa lengo la kuhamasisha pia wajiunge katika vikundi vya ujasiriamali na kuhimiza wanachama kulipa ada kwa wakati.

No comments: