Wednesday, August 10, 2016

SERIKALI YAOMBWA KUTATUA KERO YA NYUMBA ZA KUISHI ASKARI POLISI MBINGA

Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, Sixtus Mapunda akikagua nyumba ya kulala askari Polisi wageni ambayo ni chakavu na aliahidi kuifanyia ukarabati kutokana na nyumba hiyo, wakati wa masika mvua zinaponyesha huvuja na kuwafanya askari washindwe kuishi ndani ya nyumba hiyo.
Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Ramia Mganga, ambaye amesimama akitoa ufafanuazi juu ya kero mbalimbali wanazokabiliana nazo askari wake, mbele ya Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Sixtus Mapunda ambaye ameketi akiwa amevaa koti rangi ya bluu. Kikao hicho kilishirikisha baadhi ya askari wa wilaya hiyo ambao hawapo pichani.


Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa kitendo cha askari Polisi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wengi wao kuishi uraiani, kwa kiasi kikubwa kunachangia kutotimiza majukumu yao ya kazi ipasavyo, hivyo serikali imeombwa kuona uwezekano wa kutatua kero hiyo.

Aidha nyumba zilizopo ambazo baadhi yao wanaishi, zimekuwa chakavu ambapo nyakati za masika huwa zinavuja na hilo linatokana na bati zilizoezekwa kuwa na matundu yanayopitisha maji ya mvua.

Hayo yalisemwa leo na askari hao walipokuwa wakizungumza na Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Sixtus Mapunda, ambaye aliwatembelea kwa ajili ya kuzungumza nao na kusikiliza kero zao mbalimbali.

Walisema kuwa hata jengo la ofisi za kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga hali yake ni mbaya, ambapo linahitaji kufanyiwa ukarabati ili liweze kuwa kati hali nzuri.


Ramia Mganga ambaye ni Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, alisema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa Mbunge huyo ambapo alieleza kwamba kuna tatizo sugu la nyumba za kuishi askari wake, ambapo zaidi ya asilimia 80 wamekuwa wakipanga uraiani.

Mganga alifafanua kuwa askari hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu na kwamba, wanahitaji kupewa pikipiki bora za kisasa kwa ajili ya kuimarisha zoezi la ulinzi shirikishi katika kata mbalimbali wilayani Mbinga.

Kwa upande wake Mbunge, Mapunda mara baada ya kusikiliza matatizo hayo alitoa ahadi ya kukarabati jengo la kituo hicho cha Polisi kwa kulipaka rangi pamoja na nyumba moja wanayoishi askari wageni ambao huwasili kufanya kazi wilayani humo, atalifanyia ukarabati kwa kuezua bati chakavu zilizopo sasa na kuezeka bati mpya ili lisiendelee kuleta madhara kwa watumiaji hasa nyakati za masika.

“Tunathamini mchango wenu mkubwa mnaoutoa katika nchi hii, tuendelee kushirikiana kwa kuiweka Mbinga yetu wakati wote katika hali ya usalama ili wananchi waweze kufanya maendeleo yao na kukuza uchumi wetu”, alisema Mapunda.

Pamoja na mambo mengine Mbunge huyo alisema kuwa kero hizo zilizopo kwa askari wake wa wilaya ya Mbinga, atazifikisha kwa Waziri mwenye dhamana ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ikiwemo hasa juu ya suala la ujenzi wa nyumba za kuishi askari hao.

No comments: