Wednesday, August 31, 2016

BIHARAMULO WALILALAMIKIA SHIRIKA LA UGAVI WA UMEME TANZANIA

Waziri wa nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Na Mwandishi wetu,

Kagera.

BAADHI ya Wateja ambao wamelipia huduma ya kuunganishiwa nishati ya umeme majumbani kwao wilaya ya Biharamulo mkoa wa Kagera, wamelinyoshea kidole Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani humo kwa kushindwa kutimiza majukumu yake kwa wakati na kuwafanya wateja hao, wapate hasara katika kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.

Aidha imeelezwa kuwa wateja hao ambao ni wa maeneo ya mjini wamelilalamikia Shirika hilo wakidai kwamba, tokea walipolipia huduma ya kujengewa mita za umeme mwanzoni mwa mwezi wa sita mwaka huu, hakuna utekelezaji uliofanyika jambo ambalo linawafanya wawe na mashaka.

Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, walisema kuwa shughuli zao za ujasiriamali ambazo zinategemea nishati hiyo ya umeme wanashindwa kuziendesha, hivyo wanaiomba serikali itatue kero hiyo mapema ili waweze kuondokana na adha kubwa wanayoipata sasa.

Kadhalika wamemuomba Waziri mwenye dhamana, Profesa Sospeter Muhongo kuona umuhimu wa kuingilia kati ili kuweza kumaliza tatizo hilo mapema ambalo hawajui litakwisha lini.


Lazaro Daud ambaye ni mkazi wa Biharamulo mjini, akizungumza kwa niaba ya wateja wenzake alieleza kuwa kila anapokwenda kufuatilia suala hilo makao makuu ya ofisi za TANESCO wilayani humo, hakuna majibu sahihi anayopewa na kwamba wapo zaidi ya wateja 80 ambao wamekuwa wakilalamikia hali hiyo kwa muda mrefu. 

“Hata shughuli zetu za ufundi seremala zimesimama tunashindwa kuendesha viwanda vyetu vidogo vidogo kutokana na tatizo hili, hivi sasa tumekata tamaa kwani tumelipia kwa muda mrefu hakuna huduma tuliyopata”, alisema Daud.

Kwa upande wake alipohojiwa kwa njia ya simu Meneja wa shirika hilo wilayani Biharamulo, Ernest Milyango alikiri kuwepo kwa tatizo hilo huku akieleza kuwa limetokana na kukosekana kwa vifaa husika vitakavyoweza kukamilisha kazi ya kuwaunganishia umeme wateja hao majumbani kwao.

Milyango aliongeza kuwa mfumo wa manunuzi unaofanyika makao makuu ya Ofisi za TANESCO Dar es Salaam baada ya wao kupeleka orodha ya vifaa husika nao huchangia kuchelewa kuwaletea vifaa hivyo, kwani huchukua muda mrefu na kuwafanya wateja wao walalamikie hali hiyo kutokana na kukosa huduma husika.

“Nafikiri hawa wateja wetu watuvumilie kidogo, tatizo kubwa hapa ni suala la vifaa, baadhi yake vimekwisha letwa tunasubiri mpaka vikamilike ndipo wakati wowote kuanzia sasa tutaanza kazi ya kuwajengea mita za umeme”, alisema Milyango.

No comments: