Tuesday, August 2, 2016

MBINGA KUKUSANYA KODI YA ARDHI BILIONI 6.7 KILA MWAKA


Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gilbert Simya akifungua mafunzo ya siku moja hivi karibuni ya kuwajengea uwezo Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo juu ya ukusanyaji mapato na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IMEBAINISHWA kuwa, endapo halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma itapima ardhi yake katika vijiji na miji  midogo iliyopo wilayani humo, itaweza kukusanya kodi ya shilingi bilioni 6.7 kila mwaka kupitia ardhi husika iliyopimwa.

Kodi hiyo itakayokusanywa itatokana na heka 67,000 ambazo wataalamu wa ardhi wataanza kufanya kazi ya kupima wilayani humo, mapema kuanzia mwezi huu na kukamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu.

Hayo yalibainishwa na Mthamini wa ardhi halmashauri ya wilaya ya Mbinga Gabriel Kameka, alipokuwa akiwaelimisha Madiwani wa wilaya hiyo kwenye mafunzo elekezi ya siku moja yaliyolenga juu ya ukusanyaji mapato kwa halmashauri hiyo.


“Hili suala ni lazima tulivalie njuga sisi sote, tujenge ushirikiano tuweze kufanikiwa kama hatutakuwa pamoja ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu”, alisema Kameka.

Kameka alisema kuwa Madiwani wanapaswa huko waendako wakawaelimishe wananchi wao, ili zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa pasiwe na vikwazo vya aina yoyote ile.

Alisema kuwa, ikumbukwe kwamba ardhi iliyopimwa mwananchi ananufaika nayo kwa njia mbalimbali, ikiwemo kwanza ni dhamana kwake kufuatia hati aliyonayo inamfanya aweze kukopa kwenye taasisi za kifedha na kumwezesha kufanya shughuli zake za maendeleo.

Ili halmashauri iweze kupata mapato yake kupitia ardhi, alisema ni lazima ipimwe na wamiliki husika wawekeze kwenye ardhi hiyo ndipo mapato hupatikana zaidi.

Kwa upande wao Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga walisema kuwa wanafurahishwa na mipango hiyo ya kimaendeleo inayotekelezwa na wataalamu wake, hivyo waliahidi huko waendako kwenda kusimamia kikamilifu jukumu hilo walilopewa kwa kutoa elimu kwa wananchi wao ili nao waweze kushiriki kikamilifu.
 

No comments: