Tuesday, August 16, 2016

DC MBINGA APANIA KUWASAKA WAFANYABIASHARA WAJANJA WANAOTOROSHA KAHAWA



Na Kassian Nyandindi,            
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imesema kwamba, imeanza kuchukua hatua kali za kuwasaka wafanyabiashara wajanja ambao wamekuwa wakinunua na kutorosha zao la kahawa wilayani humo nyakati za usiku, kwa njia za panya kuelekea mkoani Mbeya bila kibali maalumu.

Aidha imeelezwa kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikishamiri hasa kipindi hiki cha kiangazi, pale msimu wa mavuno ya zao hilo unapofanyika ambapo wafanyabiashara hao hupita vijijini kwa wakulima na kuwarubuni kununua zao hilo kwa njia zisizo halali.

Mkuu wa wilaya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo, liloketi katika ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.


Nshenye alisema kuwa kumeshamiri tabia mbaya kwa baadhi ya wanunuzi wanao nunua zao la kahawa wilayani humo, ambapo wamekuwa wakitorosha kahawa majira ya usiku kuelekea mkoani Mbeya kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru au kodi.

“Ndugu zangu tunafanya msako mkali sasa wa kuwakamata watu wote wenye tabia hii, mfanyabiashara atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kufutiwa hata leseni ya kununua zao hili katika msimu huu”, alisema Nshenye.

Kadhalika alikemea biashara za magoma ambazo zimekuwa zikifanywa katika maeneo mbalimbali wilayani Mbinga ambapo wafanyabiashara hao wamekuwa wakimrubuni mkulima anayezalisha zao hilo, kabla ya kahawa yake kuvunwa shambani kwa mtindo wa kubadilishana na bidhaa mbalimbali.

Mkuu huyo wa wilaya alikemea vikali tabia hiyo na kuahidi kwamba atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria, pamoja na kufikishwa Mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Pamoja na mambo mengine pia aliwataka wakulima wa zao hilo kuzalisha kwa kufuata kanuni bora za kilimo, ili waweze kuzalisha kahawa yenye viwango vya hali ya juu ambavyo vinakubalika katika masoko.

Hata hivyo alisisitiza kwamba mkulima anayezalisha kahawa akizingatia kanuni za kilimo bora na kahawa yake ikawa nzuri, anaweza kujipatia soko la kuuza kahawa hiyo katika minada ya ndani na nje ya nchi.

No comments: