Friday, September 2, 2016

MKOA WA RUVUMA WATUMISHI NANE WASIMAMISHWA KAZI

Na Julius Konala,    
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma imewasimamisha kazi watumishi nane kutoka halmashauri za wilaya nne za mkoa huo ikiwemo katika wilaya zake za Tunduru, Nyasa, Mbinga na Namtumbo kwa lengo la kupisha uchunguzi baada ya kubainika wameshindwa kuzingatia weledi wa utumishi wa umma ikiwemo kufanya vitendo vya ubadhirifu wa fedha.

Hayo yalisemwa na Katibu tawala wa mkoa huo, Hassan Bendeyeko alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa mipango uliopo kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.

Bendeyeko aliwataja watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni Fortunatus Mlokozi Kakiko, ambaye ni mkaguzi wa ndani Alan Ansigali Mbunda ni Afisa ugavi na Juma Kassim Kasalo ambaye ni Mweka Hazina wote wanatoka halmashauri ya wilaya ya Tunduru.


Wengine ni Joseph Ngonyani ni mweka Hazina na Nelson Kiwehuru ambaye ni mkaguzi wa ndani wote wa kutoka halmashauri ya wilaya ya Nyasa, na kwamba Klodwick Mapunda (Mweka Hazina), Robert Mahili (Mkaguzi wa kitengo cha manunuzi) toka halmashauri ya wilaya ya Namtumbo pamoja na Emmanuel Kapinga ambaye Afisa utumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.

Alisema kuwa Afisa utumishi Kapinga amesimamishwa kutokana na uzembe wa kushindwa kusimamia zoezi la watumishi hewa, pamoja na kuwafuta watumishi sita wasiokuwa na makosa.

Katibu tawala huyo aliwataja watumishi wanaokwenda kuziba nafasi zilizoachwa wazi kwenye halmashauri hizo kuwa ni Emmanuel Nyomeye (CPA Holder) kutoka Mbinga mji na kuwa mweka hazina wilaya ya Tunduru, Paulo Humba toka Sekretarieti ya mkoa na kuwa mkuu wa kitengo cha manunuzi wilaya ya Tunduru huku Abubakari Shayo toka Namtumbo anaenda kuwa mkaguzi wa ndani wilaya ya Tunduru.

Aliendelea kuwataja wengine kuwa ni Willy Luambano kutoka Namtumbo anaenda kuwa mkaguzi wa ndani halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Pendo Nyomeye kutoka Tunduru anakwenda kufanya kazi ya kuwa mweka hazina wilaya ya Nyasa, Marcela Mapunda kutoka Tunduru kuwa, Afisa manunuzi wilaya Namtumbo, Peter Tumaini kutoka Manispaa ya Songea anaenda kuwa mweka hazina wilaya Namtumbo na Leokadia Humera kutoka Tunduru anaenda kuwa Afisa utumishi mwandamizi wilaya ya Mbinga.


Kufuatia kutokea kwa matatizo hayo, Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Bendeyeko alisema kuwa serikali imeunda kamati ya uchunguzi itakayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhandisi Ezla Daniel wa kutoka Wakala wa barabara Tanzania mkoani humo (TANROADS), Nelson Kailembo (PCCB) Norbetha Nyoni (Mkuu wa idara ya utumishi Madaba) na Adelina Komba kutoka ofisi ya Katibu tawala wa mkoa huo ambapo amedai kuwa yeyote atakayebainika kufanya makosa kwenye uchunguzi huo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

No comments: