Monday, September 5, 2016

RC RUVUMA: WATUMISHI WA SERIKALI WANAOJIONA HAWAENDANI NA KASI YA AWAMU YA TANO WAJIONDOE MAPEMA



Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

WATUMISHI wa serikali katika mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wanapaswa kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.


Kadhalika kwa wale ambao wanajiona kwamba hawawezi kuendana na kasi hiyo wameshauriwa wajiondoe mapema, kabla mkono wa sheria haujawafikia ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kuwapata hapo baadaye.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge wakati alipokuwa akizungumza na wakuu wa idara wa halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani humo, katika kikao cha kazi kilichofanyika mjini hapa.


“Tunataka kazi zote za maendeleo ya wananchi zitekelezwe kwa wakati, serikali haitaki kuona mtumishi akifanya mambo ambayo hayafanani na taratibu zake zilizopo”, alisema.

Dkt. Mahenge alieleza kuwa haipendezi kusikia katika halmashauri kunakuwa na vitendo vya ufisadi na kwamba alimuagiza Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye endapo ataliona hilo linafanyika katika wilaya yake achukue hatua haraka dhidi ya wahusika ili iweze kuwa fundisho kwa wengine.

Hata hivyo aliongeza kuwa serikali haitaki kusikia mambo yakienda hovyo badala yake imekuwa ikitaka kuona wananchi wanahudumiwa kwa misingi, sheria na taratibu zilizowekwa ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa manufaa ya jamii.

No comments: