Tuesday, September 13, 2016

AFARIKI DUNIA BAADA YA LORI KUPARAMIA NYUMBA

Na Kassian Nyandindi,          
Songea.

MTU mmoja mkazi wa kijiji cha Myangayanga Tanga pachani halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Anna Ndunguru (40) amefariki dunia baada ya lori lililokuwa limebeba shehena ya magunia ya mahindi, kuacha njia na kuparamia nyumba waliyokuwa wanaishi wakati akiwa amekaa ndani ya nyumba hiyo na wenzake wakipata mlo wa mchana.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa, lilitokea Septemba 8 mwaka huu majira ya saa 6:32 mchana ambapo lori hilo lenye namba za usajili T 231 BCH mali ya mfanyabiashara mmoja maarufu mjini hapa, Medson Ulendo lilikuwa likitokea katika kijiji cha Kilindi kata ya Matiri wilayani hapa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Festo Sangana ambaye ndiye mmiliki wa nyumba ambayo lori hilo liliparamia na kubomoa sehemu kubwa ya kuta za nyumba hiyo alisema kuwa, ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva kutokana na kuwa katika mwendo kasi ambapo gari lilimshinda kukata kona ndipo alisababisha ajali hiyo.


Sangana alifafanua kuwa baada ya dereva kusababisha tatizo hilo alitokomea kusikojulikana ambapo marehemu Ndunguru, alifikwa na umauti baada ya kukimbizwa hospitali ya misheni Litembo kutokana na kujeruhiwa vibaya mwilini mwake.

Kadhalika majeruhi wengine waliokumbwa na mkasa huo kuwa ni Frank Ndunguru (30), Shukran Sangana (26) na mtoto mmoja mdogo aliyetajwa kwa jina la Sabina Komba mwenye umri wa mwaka mmoja, wote wakazi wa Myangayanga Tanga pachani mjini hapa.

Mganga mfawidhi hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga Dkt. Robert Elisha alikiri kuwapokea majeruhi hao na kuongeza kuwa hali zao zinaendelea vizuri na kwamba Anna Ndunguru, alipewa rufaa ya kupelekwa hospitali ya Misheni Litembo kwa matibabu zaidi kutokana na kuwa na hali mbaya ambako amepoteza maisha.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na Jeshi hilo linamshikilia dereva wa gari hilo Erick Mbelle mkazi wa Tangi la maji Mbinga mjini, ambaye anadaiwa kuendesha huku akiwa amelewa ndio maana alisababisha ajali hiyo na kwamba wakati wowote atafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

“Huyu dereva baada ya kusababisha ajali hii alikimbia katika eneo la tukio hakuweza kupatikana, baada ya siku chache kupita alijileta mwenyewe kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga ndipo tulipomkamata na sasa tunamshikilia ili tuweze kumfikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria”, alisema Mwombeji.


No comments: