Sunday, September 25, 2016

WATUMISHI WA SERIKALI RUVUMA WENYE KUFANYA KAZI KWA MAZOEA KUKIONA CHAMTEMAKUNI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo katika sehemu ya vikao vyake vya kikazi na chama mkoani hapa.
Na Julius Konala,       
Songea.

WATUMISHI wa Serikali waliopo katika sekta mbalimbali mkoani Ruvuma, wametakiwa kujiepusha na vitendo vya utoaji huduma kwa wananchi kwa mtindo wa upendeleo au kujenga tabia ya kuendekeza vitendo vya rushwa, itikadi za dini na ukabila.

Aidha kwa mtumishi yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi, ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema hayo juzi alipokuwa akizindua Baraza la Wafanyakazi la watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Ikulu ndogo mjini Songea.

Dkt. Mahenge alieleza kuwa serikali haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi yeyote atakayebainika kwenda kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma badala yake wanapaswa kuwahudumia Watanzania wote kwa kufuata usawa.


“Nawataka watumishi wote ndani ya mkoa wangu endeleeni kuunga mkono kauli mbiu ya Rais wa awamu ya tano Dkt. John Magufuli ya Hapa kazi tu, kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na maarifa acheni kutumia muda mwingi mnapokuwa ofisini kuchati kwenye mitandao badala ya kufanya kazi, malizeni kero za wananchi kwa wakati”, alisema Dkt. Mahenge.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la watumishi wa Ofisi hiyo ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko ambaye pia ni Katibu tawala wa mkoa huo alisema kuwa lengo la kuundwa kwa baraza hilo ni kuboresha utendaji kazi, mahali pa kazi na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa umma ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi  wa Serikali na Afya (TUGHE) mkoani Ruvuma, Denice Tosiri aliwataka wajumbe wa baraza hilo kutambua kuwa wajibu wao mkubwa ni kutoa changamoto, kuzungumzia kero, kuwepo kwa ushirikiano kati ya watumishi na waajiri, kuishauri serikali juu ya ufanisi mahali pa kazi, kuboresha maslahi yao kazini, kupandishwa vyeo na kutoa ushauri katika matumizi ya fedha.

Tosiri aliongeza kuwa wajumbe hao wanatakiwa pia kutambua kuwa wao ni mabalozi wanaowakilisha wenzao, hivyo pale wanaposikia manung’uniko na migogoro sehemu za kazi wanapaswa kutatua haraka iwezekanavyo huku wakitakiwa kuboresha huduma kwa wateja, kuonyesha nidhamu pamoja na kutunza siri za ofisi.

No comments: