Sunday, September 25, 2016

DC SONGEA AWAKALIA KOONI WASIOFANYA USAFI

Na Kassian Nyandindi,        
Songea.

AGIZO limetolewa kwa Watendaji wote wa Halmashauri za wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kuhakikisha kwamba wanawapiga faini wananchi ambao wataonekana kutotii amri ya kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili iweze kuwa fundisho kwa wengine na kuleta mabadiliko chanya, kwa jamii kujenga tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao.

Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa mtaa wa Miembeni kata ya Bombambili mjini hapa, ambako shughuli za usafi wa mazingira kiwilaya zilikuwa zikifanyika na kuongozwa naye.

Kwa ujumla wilaya hiyo inaundwa na halmashauri tatu ambazo ni Manispaa ya Songea, halmashauri ya wilaya ya Songea na ile ya Madaba.

Mgema alisema kuwa watu wote ambao hawataki kufanya usafi wa mazingira kuanzia sasa watozwe faini ya shilingi 50,000 na kwamba anataka ripoti ya watu hao pale wanapotozwa ifikishwe ofisini kwake haraka, ili aweze kutambua ni nani wenye tabia ya kugoma kufanya usafi ili waweze kuchukuliwa hatua zaidi.


Alifafanua kuwa taarifa alizonazo ni kwamba, kuna baadhi ya wakazi waliopo katika mitaa mbalimbali ndani ya wilaya hizo wakiwemo pia wafanyabiashara wamekuwa na mazoea ya kugoma kujitokeza kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, hali ambayo inawakatisha tamaa wengine wenye moyo wa kutekeleza jambo hilo muhimu.

“Natoa agizo kwa Ofisa afya wa halmashauri ya Manispaa Songea na timu yote ya ya uongozi wa kata na mitaa, hakikisheni wale wote ambao hawashiriki kufanya usafi wanakamatwa na kupigwa faini ya shilingi 50,000 kila mmoja”, alisisitiza Mgema.

Kadhalika aliongeza kuwa, jukumu la kufanya usafi ni la kila mmoja ili kuweza kuepukana na magonjwa yanayotokana na uchafu kutokana na mazingira kuwa na hali mbaya ya uchafu.

Vilevile kwa upande wake Ofisa afya wa Manispaa hiyo, Maxensius Mahundi alimhakikishia Mkuu huyo wa wilaya ya Songea kwamba idara yake imejipanga kikamilifu katika kusimamia masuala ya usafi wa mazingira kwa vitendo na kwamba, tayari wamenunua magari matatu ya kuzolea taka ambayo yatasaidia kupunguza kero ya kuzoa taka zitakazolundikana katika maghuba.


Mahundi aliongeza kuwa katika kukabiliana na watu wanaochafua mazingira kila kata itatoa vijana kumi, ambao watapewa mafunzo juu ya kusimamia masuala ya usafi kwenye mitaa na kata zao.

No comments: