Wednesday, September 21, 2016

CCM WAPONGEZA UJENZI WA BARABARA NYANDA ZA JUU KUSINI

Na Muhidin Amri,          
Tunduru.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kimeishukuru serikali kwa kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa wananchi wa wilaya hiyo na ukanda wote wa mikoa ya nyanda za juu Kusini.

Chama hicho kimesema kwamba kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutoka Songea hadi wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, kupitia Tunduru ambayo ilikuwa na mateso makubwa kwa wananchi kutokana na kupitika kwa shida nyakati za masika hivi sasa ujenzi huo utasaidia kufungua fursa za kiuchumi, mawasiliano na hata kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Hayo yalisemwa jana mjini  hapa na Katibu wa CCM wa wilaya hiyo Mohamed Lawa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya hatua ambazo serikali ya awamu ya tano imeanza kutekeleza kwa wananchi wa wilaya ya Tunduru.


Lawa alisema kuwa mbali na ujenzi wa barabara hiyo pia serikali imekamilisha mradi wa ujenzi wa njia kuu za kusambaza nishati ya umeme katika vijiji 19 jimbo la Tunduru Kaskazini ambapo mradi huo unaendelea kujengwa kwa vijiji vyote vilivyopo pia katika jimbo la Tunduru Kusini, hivyo kuanza kuleta matumaini kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Alifafanua kuwa kukamilika kwa mradi wa barabara hiyo kumesaidia kuongezeka kwa shughuli za utalii kwani hata Watalii wengi kutoka nje na ndani ya mkoa wa Ruvuma, wameanza kwenda kwa wingi hasa ikizingatia kuwa wilaya hiyo imezungukwa na hifadhi ya taifa ya Selou, ambapo wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo kujenga nyumba na hoteli za kisasa kwa ajili ya kukuza uchumi wao.

“Kutokana na kufunguka kwa barabara hii ni matumaini yetu watu wengi zaidi watafika hapa wilayani kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hivyo tunawataka wananchi kuongeza uzalishaji wa chakula mashambani na kujiepusha kuuza ardhi yao hovyo kwa wageni badala yake wawekeze kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye”, alisema Lawa.


No comments: