Saturday, September 17, 2016

BENKI YA NMB YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE WAJASIRIAMALI WAPIGWA MSASA SONGEA

Meneja wa benki ya Nmb tawi la Songea mkoani Ruvuma, Colman Kiwia akizungumza na Wajasiriamali wadogo na wa kati katika kikao kati ya benki hiyo na Wajasiriamali hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Heritage Cottage mjini Songea.

Mjasiriamali mdogo kutoka wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Sarah Komba ambaye ni mteja wa benki ya NMB akizungumza wakati wa kikao hicho cha pamoja kati ya wateja wa benki hiyo na uongozi wa NMB tawi la Songea pamoja na wa kutoka makao makuu ya Kanda Mtwara.
Na Muhidin Amri,    
Songea.

WAJASIRIAMALI wadogo na wakati kutoka katika wilaya tano za mkoa wa Ruvuma, wameipongeza benki ya NMB  kwa kuwa na mipango thabiti inayolenga kupunguza umaskini kwa wananchi wengi, ikiwemo kutoa mikopo yenye riba nafuu hatua ambayo itasaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Pongezi hizo zilitolewa na Wajasiriamali hao wa kutoka wilaya ya Tunduru, Namtumbo, Mbinga, Songea na Nyasa mkoani humo wakati walipokuwa juzi kwenye kikao chao na uongozi wa benki hiyo Kanda ya kusini, kinachojulikana kwa jina la NMB BUSINESS CLUB ambacho kilihudhuriwa pia na maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania, Jeshi la zimamoto na Maafisa biashara wa Manispaa ya Songea  katia ukumbi wa Heritage Cottage mjini hapa.

Aidha wameiomba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Magufuli kuiunga mkono benki hiyo ambayo imeonekana kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wengi, hasa wenye kipato kidogo ambao wameanza kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki ya NMB ikiwemo zile za mikopo ambayo huwawezesha kuanzisha biashara ndogo ndogo na shughuli nyingine za kimaendeleo.


Katika hatua nyingine, baadhi ya  wajasiriamali hao wilayani Songea wameuomba uongozi wa Manispaa ya Songea kuondoa kiwango cha  fedha inachotoza kwa wananchi wanaotaka kuchukua mkopo na kutumia hati zao za nyumba kama dhamana ambazo hupelekwa idara ya ardhi kwa ajili ya uhakiki kwani tozo hizo humuumiza mwananchi wa kawaida na kukwamisha malengo yake.

Walisema kuwa Manispaa hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikiwatoza wananchi shilingi 40,000 kila anayehitaji kupata mkopo kutoka benki au taasisi yoyote ile ya kifedha jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa kwani mtu anapohitaji mkopo benki ni lazima alipie fedha hizo.

Walifafanua kuwa utaratibu huo haufai na kwamba hauwezi kumsaidia mwananchi wa kawaida kumuondoa katika janga la umaskini, badala yake wameshauri Manispaa kutafuta vyanzo mbadala vya mapato kuliko kuendelea kuwanyonya watu maskini wanaokabiliwa na changamoto nyingi za maisha.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Sara Komba alisema kuwa kuna umuhimu sasa kwa serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato na kuachana na vile vinavyomuumiza mwananchi ambaye hutafuta namna ya kujikwamua na umaskini.

Kwa upande wake Meneja wa benki ya NMB tawi la Songea, Colman Kiwia alisema kuwa licha ya mafanikio makubwa iliyoyapata benki hiyo hata hivyo kuna changamoto kubwa  iliyopo kutoka kwa baadhi ya wateja wanaochukua mikopo kushindwa kuirejesha kwa wakati na waombaji wapya kukosa sifa ya kupata mkopo pale wanapotaka kutumia ardhi zao ambazo hazijapimwa kutokana na kukosekana kwa hati miliki.


Hata hivyo alisema kuwa wakati umefika sasa kwa wananchi wa Songea kuona umuhimu wa kupima maeneo yao  ili waweze kupata hati hizo miliki, ambazo zitawasaidia kwa ajili ya kupata mikopo kutoka katika taasisi za kifedha na kuboresha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

No comments: