Monday, September 5, 2016

MAKAMPUNI YA KAHAWA MBINGA YAPEWA SIKU 14 KUKAMILISHA MALIPO YA WAKULIMA

Cosmas Nshenye, Mkuu wa wilaya ya Mbinga.


Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye ametoa amri kwa Makampuni yanayonunua kahawa wilayani humo kuhakikisha kwamba ndani ya siku 14 kuanzia sasa, yawe yamekamilisha malipo ya awamu ya pili ya fedha za wakulima wa kahawa na kwamba kampuni itakayoshindwa kutekeleza amri hiyo itachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Aidha ametoa agizo kwa wafanyabiashara wote wanaojishughulisha na biashara ya zao hilo, kuandaa takwimu za malipo na mauzo ya kahawa ambapo mara baada ya msimu wa mauzo kwisha, takwimu hizo ziwasilishwe ofisini kwake ili serikali iweze kuzifanyia kazi.

Nshenye alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha Wadau wa kahawa wilayani hapa, ambacho kilishirikisha wafanyabiashara, vikundi vya wakulima na makampuni ambayo hujishughulisha na ununuzi wa zao hilo wilayani humo.

“Ndugu zangu hili sio ombi, takwimu hizi tukishazipata zitaisaidia serikali kutambua ni nani ameuza kahawa hasa kwa wale watu wajanja wasiokuwa na mashamba, ambao hupita vijijini kwa wakulima na kuendelea kumnyonya mkulima abaki kuwa maskini’, alisema Nshenye.


Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alisisitiza kuwa ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kupita majumbani kwa mkulima na kununua kahawa badala yake watumie vituo maalumu vilivyowekwa na serikali, kwa ajili ya kununulia zao hilo.

Alisema kuwa haitaji kuona mtu au kampuni inakiuka taratibu na sheria zilizowekwa na serikali na kwamba kwa atakayeona masharti yaliyowekwa hawezi kuyafuata, ajiondoe mapema kabla mkono wa sheria haujamfikia na kujikuta yupo mahali pabaya.

Vilevile aliiagiza Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Kanda ya Ruvuma, kuhakikisha kwamba inafuatilia mikataba yote ya makampuni yanayofanyabiashara ya kahawa wilayani humo na mkulima, ili kujiridhisha kama mikataba hiyo inamsaidia mkulima huyo na ofisi yake ipewe majibu ndani ya siku 14 kuanzia sasa.

Hata hivyo aliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuweza kubaini mikataba yote yenye utata ambayo haimsaidii mkulima, ili serikali iweze kuingilia kati na kuchukua hatua husika ya kurejesha haki zote za mkulima ikiwemo kampuni au mfanyabiashara husika kuwajibishwa kwa kufutiwa leseni yake ya biashara ya kahawa.

No comments: