Saturday, September 24, 2016

GAMA: UMEME GRIDI YA TAIFA SONGEA KUUNGANISHWA 2018

Na Kassian Nyandindi,           
Songea.

IMEELEZWA kwamba ifikapo mwaka 2018, mji wa Songea ambao ni makao makuu ya mkoa wa Ruvuma unatarajiwa kuunganishwa na umeme wa gridi ya taifa kutoka Makambako mkoa wa Njombe.

Leonidas Gama.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Songea mjini, Leonidas Gama alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Misufuni mjini hapa na kuongeza kuwa serikali imekwisha anza mchakato wa kukamilisha kazi hiyo, ili utekelezaji wake uweze kuanza mara moja.

“Nataka kuwahakikishia kwamba mkandarasi ameanza kazi mwaka huu kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa kuweza kuleta umeme huu wa gridi ya taifa, kutoka Makambako ambao utapitia Madaba hadi Songea mjini makao makuu ya mkoa wetu wa Ruvuma”, alisema Gama.


Alisema kuwa umeme huo utakapokuwa umefika Songea fursa nyingi za uwekezaji zitakuwepo, ikiwemo ujenzi wa viwanda vikubwa vitakavyoweza kutoa ajira kwa watu wengi hususani vijana na kuweza kuongeza kasi ya kukua kiuchumi.

Mji wa Songea kwa miaka mingi kutokana na kutokuwepo umeme wa uhakika hali hiyo inasababisha hadi sasa kutokuwepo kwa viwanda hivyo, jambo ambalo linachelewesha hata kukua kwa maendeleo ya wananchi na mkoa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Mbunge huyo alisema kuwa serikali inatarajia kujenga pia hospitali kubwa ya kisasa, yenye viwango vya kukidhi matibabu ya hali ya juu katika eneo la Mwengemshindo Manispaa ya Songea mkoani humo.


Gama alisema kuwa tayari wataalamu kutoka Wizara ya wa afya hapa nchini, wamekagua katika eneo hilo itakapojengwa hospitali na kwamba ujenzi wake utakapokamilika itakuwa mkombozi mkubwa, hasa kwa wananchi waishio nyanda za juu Kusini kwa kile alichoeleza kuwa hawatakuwa na sababu tena ya wagonjwa kupewa rufaa kwenda hospitali ya taifa Muhimbili.

No comments: