Tuesday, September 13, 2016

WATENDAJI TUNDURU WATAKIWA KUTEKELEZA MAAGIZO WALIYOPEWA

Na Kassian Nyandindi,             
Tunduru.

MAAFISA Watendaji wa kata katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wametakiwa kuhakikisha kwamba zoezi la kufyatua tofari kwa kila kijiji wilayani humo linatakiwa liwe limekamilika mapema iwezekanavyo Septemba 15 mwaka huu.

Aidha wamesisitizwa kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao ya utendaji kazi, ambapo kila mnunuzi wa mazao mchanganyiko anatakiwa kuwa na kibali cha ununuzi kutoka halmashauri ya wilaya hiyo na leseni hai ya biashara husika.

Agizo hilo lilitolewa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Abdallah Mussa alipokuwa katika kikao cha kazi juzi akizungumza na Watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo mjini hapa.


Pia Mussa alipiga marufuku kwa wanunuzi wa mazao hayo kutumia mizani ya saa kutokana na udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wanunuzi kwa kuweka vitu vinavyoongeza uzito kama vile mchanga, misumari na sumaku hivyo kuwaibia wakulima.

“Tutazunguka kila kijiji, kata, mtaa na vitongoji vyote vilivyopo hapa wilayani nikikuta mnunuzi anatumia mizani ya saa mtendaji kazi hakuna, sitaki kuona mtumishi katika wilaya hii anazembea katika majukumu yake ya kazi”, alisisitiza Mussa.

Hata hivyo watendaji hao amewapatia muda wa wiki mbili, waainishe maghala yote mabovu kupitia viongozi wa vijiji ili halmashauri ya wilaya ya Tunduru iweze kupata taarifa ya tathimini ya pamoja ni jinsi gani nguvu ya wananchi inaweza kutumika, katika kukarabati maghala hayo ambayo ni chakavu.



No comments: