Monday, September 19, 2016

RC RUVUMA AWATAKA WADAU WA MAENDELEO KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

Na Kassian Nyandindi,           
Namtumbo.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amewataka Wadau mbalimbali katika mkoa huo kuona umuhimu wa kuendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli za maendeleo ya wananchi, ili kuweza kuharakisha ukuaji wa uchumi ndani ya mkoa huo.

Dkt. Mahenge alitoa kauli hiyo juzi mjini Namtumbo mkoani hapa, wakati alipokuwa akifungua kikao maalumu kwa ajili ya uanzishaji wa Benki ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kilichofanyika mjini hapa.

Alisema kuwa kuazishwa kwa benki hiyo ni agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, katika kikao chake na Wakuu wa mikoa mjini Dodoma kwamba kila mkoa unapaswa kuona umuhimu wa kuanzisha  benki ya wananchi ili iweze kusaidia kukua kwa uchumi na kusogeza huduma za kifedha kwa karibu zaidi katika eneo husika.


Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kupitia fursa hiyo, kipato cha mwananchi mmoja mmoja kitaongezeka kutoka wastani wa shilingi milioni 2,082,167 kwa  takwimu za mwaka 2014 hadi kufikia wastani wa shilingi milioni 3,257,368 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema zaidi ya asilimia 90 ya  uchumi wa mkoa wa Ruvuma, unategemea kilimo kwani mkoa huo ni miongoni mwa mikoa michache yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya aina mbalimbali ya chakula na biashara, ambapo uzalishaji wake hutegemea kwa kiasi kikubwa nguvu ya mwananchi mmoja mmoja ambapo serikali imekuwa ikisaidia kutoa pembejeo za kilimo kwa mfumo wa ruzuku kwa mazao ya nafaka.

Licha ya mafanikio hayo aliongeza kuwa bado wakulima wa mkoa huo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kukosa mitaji ya kuendeshea shughuli zao za kilimo, ambapo hali hiyo inasababishwa na masharti magumu ya mikopo itolewayo na taasisi za kifedha na kwamba hivi sasa hapa Ruvuma kuna benki moja tu ya wananchi iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani humo, ambayo huwasaidia wakulima katika kuinua sekta ya kilimo kwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara, ambayo ni Mbinga Community Bank (MCB).


Kwa mujibu wa Dkt. Mahenge alieleza kuwa benki hiyo ndiyo imekuwa ikiwasaidia wakulima wengi kupata mikopo, yenye gharama nafuu ya pembejeo za kilimo na shughuli nyingine za ujasiriamali katika kuendesha maisha yao.

No comments: