Sunday, September 11, 2016

SASAWALA NAMTUMBO HAWANA VYOO BORA VYA KUJISAIDIA WANAFUNZI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akiwa katika ziara yake ya kikazi juzi wilayani Namtumbo. (Picha na Yeremias Ngerangera)
Na Julius Konala,      
Namtumbo.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge, amefanya ziara ya kushitukiza katika shule ya msingi Sasawala iliyopo wilayani Namtumbo mkoani humo na kubaini shule hiyo kuwa na ukosefu wa vyoo bora vya kisasa kwa ajili ya kujisaidia wanafunzi.

Mahenge alikumbana na changamoto hiyo juzi baada ya kufanya ziara hiyo iliyolenga kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kuhimiza suala la ufyatuaji wa matofali 100,000 kwa kila kijiji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati, madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu pamoja na vyumba vya maabara.

Alisema kuwa hali hiyo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kwa wanafunzi wa shule hiyo ambapo ameutaka uongozi wa wilaya hiyo, kuhakikisha kwamba unaanza mchakato wa ujenzi wa vyoo shuleni hapo haraka iwezekanavyo ili kuweza kunusuru afya za watoto hao.

“Kwa kweli nimesikitishwa sana kuona karne hii ya leo bado kuna baadhi ya shule za msingi wanafunzi wake, wanatumia vyoo vilivyojengwa kwa kuzungushiwa nyasi na havina milango jambo hili nasema ni udhalilishaji mkubwa hasa kwa watoto wa kike”, alisema Dkt. Mahenge.


Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa mkoa amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Luckness Amlima na Mkurugenzi wake wa halmashauri ya wilaya hiyo, Christopher Kilungu kuhakikisha kwamba wanafanya ziara ya kutembelea shule zote za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo walimu na wanafunzi.

“Tembeleeni shule hizi mtaweza kuwa na takwimu za maabara, matundu ya vyoo, madarasa na nyumba za walimu katika kila shule, badala ya kusubiri taarifa ziwafikie mezani kutoka kwa wataalamu wenu”, alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Amlima alisema kuwa amepokea maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu huyo wa mkoa na kuahidi kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo huku akiwataka wananchi kushirikiana na serikali, katika shughuli za maendeleo ili ifikapo mwezi Novemba mwaka huu ujenzi huo wa vyoo uwe umekamilika.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Kilungu alisema kuwa suala la ujenzi wa vyoo katika shule za msingi na sekondari wilayani humo tayari upo katika mpango, hivyo kinachoendelea ni kuanza hatua ya utekelezaji wa haraka ikiwemo kuwashirikisha wananchi katika kuchangia nguvu zao na serikali kutoa vifaa vya kiwandani.

No comments: