Thursday, September 15, 2016

MBINGA YATENGA MBEGU TANI SITA ZA MBAAZI KWA AJILI YA WAKULIMA

Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

HALMASHAURI ya  wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetenga mbegu tani sita za zao la mbaazi kwa wakulima wa wilaya hiyo sawa na kilo 6,000 kwa lengo la kuwataka wakulima hao, kufufua zao hilo ili waweze kuinua uchumi wao na kuacha kutegemea zaidi zao la kahawa na mahindi.

Kwa mujibu wa Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Yohanes Nyoni alisema kuwa kilo hizo 6,000 zitapandwa katika ekari 2,000 ambapo kila ekari moja itapandwa kilo tatu za mbegu za mbaazi na kwamba zitasambazwa katika maeneo yanayostawi vizuri ili wakulima waanze kuzalisha katika msimu ujao wa 2016/2017.

Nyoni alisema kuwa usambazaji wa mbegu hizo kwa wakulima wilayani Mbinga ni mkakati pia wa kuboresha na kuongeza vyanzo vya mapato, hususani kwenye mazao ya chakula na biashara yanayozalishwa wilayani humo.


“Tukizalisha mazao mengi ya aina mbalimbali hapa kwetu, hasa kwa mazao haya ya chakula na biashara tutaiwezesha halmashauri yetu kupata fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wetu”, alisema Nyoni.

Ofisa kilimo huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika kuhakikisha kwamba zao la mbaazi linaleta tija na kusaidia kukua kwa uchumi wa wilaya pamoja na kubadili maisha ya wananchi wake, halmashauri hiyo kupitia idara yake ya kilimo imekwisha fanya utafiti kwamba ni maeneo gani yanayostawi  vizuri zao hilo ili kuweza kupata mavuno mengi.

Alisisitiza kuwa wakulima hupewa mafunzo ya kuzalisha mbaazi kwa kufuata kanuni za kilimo bora na kwamba, endapo mkulima atazingatia kanuni hizo ekari moja anao uwezo wa kuvuna gunia nane hadi 10.

“Gunia moja huwa na uzito wa kilo 90 ambapo kilo moja ya mbaazi huuzwa kwa shilingi 3,500 hadi 4,000 kulingana na hali ya soko, hivyo tunawashauri wakulima wetu wazalishe kwa wingi ili waweze kuwa na kipato zaidi”, alisema.

Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa mbali na halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuwapatia wakulima hao mbegu hizo, pia itatoa pembejeo za kilimo ikiwemo madawa na mbolea pamoja na kuwatafutia soko la uhakika kwa ajili ya kuuza mazao yao.


Katika hatua nyingine Nyoni amewaonya wanunuzi wa mazao ya chakula na biashara wanaokwenda wilayani humo, kufuata taratibu zilizopo ikiwemo kununua mazao katika vituo maalumu vilivyotengwa na halmashauri na sio kwenda moja kwa moja shambani kwa mkulima kwani kitendo hicho kimekuwa kikisababisha kuwanyonya na kuwatia hasara wakulima.

No comments: