Thursday, September 8, 2016

WANUSURIKA KUPOTEZA MAISHA BAADA YA LORI KUPARAMIA NYUMBANI KWAO


Lori hili lenye namba za usajili T 231 BCH ndilo ambalo limesababisha maafa hayo. (Picha na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

WATU watatu wakazi wa Tanga pachani kata ya Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wamenusurika kupoteza maisha yao baada ya lori lililokuwa limebeba shehena ya magunia ya mahindi, kuacha njia na kuparamia nyumba wakati wakiwa wamekaa ndani ya nyumba hiyo wakipata mlo wa mchana.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa lilitokea Septemba 8 mwaka huu, majira ya saa 6:32 mchana ambapo lori hilo lenye namba za usajili T 231 BCH mali ya Mfanya biashara mmoja maarufu mjini hapa, Medson Ulendo lilikuwa likitokea katika kijiji cha Kilindi kata ya Matiri wilayani hapa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Festo Sangana ambaye ndiye mmiliki wa nyumba ambayo lori hilo liliparamia na kubomoa sehemu kubwa ya kuta za nyumba hiyo alisema kuwa, ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva kutokana na kuwa katika mwendo kasi ambapo gari lilimshinda kukata kona ndipo alisababisha ajali hiyo.


Sangana alifafanua kuwa baada ya dereva kusababisha hali hiyo alitokomea kusikojulikana na kwamba walitoa taarifa kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga ambapo askari walikwenda huko na kushuhudia uharibifu uliofanyika.

Mwandishi wa gazeti hili ambaye alikuwasili katika eneo la tukio hilo, alishuhudia majeruhi wanne ambao raia wema walijitokeza na kuwakimbiza katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga ili kuweza kunusuru maisha yao.

Kadhalika majeruhi hao ambao ni Anna Ndunguru (40), Frank Ndunguru (30), Shukran Sangana (26) na mtoto mmoja mdogo aliyetajwa kwa jina la Sabina Komba mwenye umri wa mwaka mmoja, wote wakazi wa Tanga pachani mjini hapa.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya halmashauri ya mji wa Mbinga Dkt. Robert Elisha alikiri kuwapokea majeruhi hao na kuongeza kuwa watatu kati ya hao hali zao zinaendelea vizuri na kwamba Anna Ndunguru amepewa rufaa ya kupelekwa hospitali ya Misheni Peramiho kwa matibabu zaidi kutokana na kuwa na hali mbaya.


Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo jeshi hilo linamsaka dereva wa gari hilo Erick Mbelle mkazi wa Tangi la maji mjini hapa, ambaye anadaiwa kuendesha huku akiwa amelewa ndio maana alisababisha ajali hiyo.

No comments: