Sunday, September 11, 2016

WAKULIMA RUVUMA WAFURAHIA UTARATIBU WA UNUNUZI MAHINDI ULIOPANGWA NA SERIKALI

Na Julius Konala,         
Songea.

BAADHI ya wakulima mkoani Ruvuma, wamefurahia utaratibu uliopangwa na serikali kupitia kitengo chake cha Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula Tanzania (NFRA) kanda ya Songea mkoani humo, kwa kufungua vituo vya ununuzi wa mahindi katika vijiji mbalimbali kwa kile walichoeleza kuwa kufanya hivyo kumeweza kutoa fursa kwa wakulima wadogo wadogo, kuuza mazao yao pamoja na kuondoa malalamiko yasiyokuwa na msingi.

Pongezi hizo zilitolewa na wakulima hao mwishoni mwa wiki mbele ya Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa katika ziara yake ya kikazi kutembelea vituo hivyo vilivyotengwa kwa ajili ya ununuzi wa mahindi msimu wa mwaka 2016/2017 mkoani hapa.

Walisema kuwa awali utaratibu huo ulikuwa ukiwanufaisha walanguzi na wafanyabiashara wakubwa na sio kwa wakulima wadogo kama ilivyo sasa.


Akizungumza na wakulima hao kwenye vituo mbalimbali vya kununulia mahindi hapa mkoani Ruvuma, Meneja wa NFRA kanda ya Songea Majuto Chabruma alisema kuwa msimu wa mwaka 2016/2017 kanda hiyo imepangiwa kununua tani 20,000 za mahindi, ambazo zitagawanywa kwa kila wilaya kutokana na idadi ya uzalishaji husika.

Chabruma amewataka wakulima hao kuuza mahindi yao kwa kuzingatia ubora na kwamba amezitaja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni kuuziwa mahindi yenye takataka, uhaba wa fedha pamoja na wakulima kulalamikia utaratibu wa kupima gunia kumi kumi.

Akihutubia kwenye vituo hivyo vya ununuzi wa mahindi, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amewataka wakulima hao kujiwekea akiba ya chakula badala ya kuuza mahindi yote na kwamba amewaagiza Wakuu wa wilaya zote mkoani humo, kufanya ukaguzi wa nyumba hadi nyumba kwa lengo la kuwabaini waliouza ziada ya chakula walichojiwekea.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa uendeshaji Wakala wa taifa hifadhi ya chakula katika kanda hiyo, Nicodemus Massao alisema kuwa wanampango wa kupanua wigo katika kuboresha huduma zake ikiwemo pamoja na kujenga kiwanda cha nafaka, maabara ya kisasa na uzio kuzunguka kituo hicho.

No comments: