Tuesday, September 6, 2016

UPIMAJI MASHAMBA YA KAHAWA MBINGA KUWANEEMESHA WAKULIMA

Na Kassian Nyandindi,            
Mbinga.

MASHAMBA ya wakulima wanaozalisha zao la kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, yamewekwa katika mpango wa kupimwa kisheria ili wakulima hao waweze kuwa na hati miliki za kimila, ambazo zitawasaidia waweze kusonga mbele kimaendeleo.

Aidha upimaji huo wa mashamba unalenga pia kuifanya serikali iweze kutambua ni wakulima wangapi wilayani humo wanamashamba ya kahawa, ili hapo baadaye iweze kutengeneza takwimu zake halisi zitakazowatambua wazalishaji wake wa zao hilo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Gombo Samandito alipokuwa akitolea ufafanuzi juu ya faida za upimaji ardhi katika kikao cha wadau wa kahawa kilichofanyika juzi mjini hapa.


Samandito alifafanua kuwa upimaji huo utaenda sambamba na kupimwa ardhi inayozalishwa mazao mengine pamoja na ile ya makazi ya watu, ikiwa ni lengo la kuhakikisha kwamba kila mwananchi anayemiliki ardhi anakuwa na hati miliki ya kimila ambayo itaweza kumsaidia katika kuinua uchumi wake.

“Wadau wetu wa kahawa kuna umuhimu mkubwa wa kupima ardhi yenu, zoezi hili tunatarajia kulianza wakati wowote kuanzia sasa mara baada ya taratibu husika kukamilika, hivyo tutakapoanza kufanya kazi hii tunahitaji ushirikiano wenu wa kutosha”, alisisitiza Samandito.

Pamoja na mambo mengine, kwa mujibu wa taarifa ya maendeleo ya zao la kahawa wilayani Mbinga, zinaeleza kuwa katika msimu wa mavuno mwaka 2015/2016 jumla ya tani 15,000 za kahawa kavu zilizalishwa kutoka kwa wakulima wa zao hilo.

Vilevile katika kipindi cha mwaka 2016/2017 wilaya hiyo inatarajia kuvuna tani 13,000 na kwamba upungufu huo wa uzalishaji, unatokana na mikahawa mingi kuzaa kwa wingi msimu uliopita pamoja na kushambuliwa na wadudu waharibifu aina ya Vidung’ata.

Hata hivyo tokea msimu wa kahawa ufunguliwe Julai Mosi mwaka huu, mpaka sasa jumla ya tani milioni 3,737171.1 zimekusanywa na kukobolewa katika viwanda vya kukoboa kahawa vilivyopo wilayani humo.


No comments: