Monday, September 5, 2016

DOKTA MAHENGE: HAKIKISHENI HUDUMA YA MAJI SAFI NA SALAMA INATOSHELEZA KATIKA MJI WA MBINGA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo katika kikao cha kazi kilichofanyika mjini hapa, wakati alipokuwa akizungumza juzi na Wakuu wa idara wa halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani humo.


Na Kassian Nyandindi,              
Mbinga.

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) halmashauri ya mji wa Mbinga mkoa wa Ruvuma, imetakiwa ihakikishe kwamba huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama katika mji huo inatosheleza wakati wote kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akizungumza na wakuu wa idara wa wilaya hiyo katika kikao cha kazi kilichofanyika mjini hapa.

“Nataka kuona maji yanatosheleza katika mji huu ili tuweze kuwaondolea adha wananchi wetu kutafuta maji umbali mrefu, boresheni mindombinu ya maji na kukusanya madeni ya ankra za maji kwa wakati”, alisisitiza Dkt. Mahenge.


Mkuu huyo wa mkoa aliagiza pia kwa kuutaka uongozi wa Mamlaka hiyo kutunza vyanzo vyake vya maji kwa kuwaondoa watu wote waliovamia vyanzo hivyo, ili visiweze kukauka na kuleta madhara makubwa ya kutopatikana maji ya kutosha katika mji huo.

Alisema anataka kuona mkoa wa Ruvuma katika maeneo mbalimbali mazingira yanatunzwa vizuri ili uoto wa asili uliopo sasa, uweze kuwa endelevu kwa faida hata ya viumbe hai ambavyo huishi katika misitu na maeneo mengine.

“Tunataka mkoa wetu wananchi waheshimu suala la utunzaji wa mazingira, vinginevyo pale nitakapoona kuna tofauti fulani viongozi wa wilaya jambo hili litawagharimu”, alisema.

Hata hivyo Dkt. Mahenge alikemea vitendo vya ukataji miti hovyo na uchomaji moto misitu hiyo ambapo amewataka viongozi husika, kusimamia jambo hilo kwa kuhakikisha watu hawafanyi uharibu huo ili mazingira yasiweze kuharibiwa na kuleta madhara makubwa hapo baadaye.

No comments: