Saturday, September 10, 2016

POLISI SONGEA WAMSAKA MWENDESHA BODABODA ALIYEUA MWANAFUNZI

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka mwendesha bodaboda ambaye jina lake limehifadhiwa kwa tuhuma za kumgonga mtembea kwa miguu, ambaye ni Mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Lilondo halmashauri ya wilaya ya Madaba, Martha Mussa (7) na kumsababishia kifo papo hapo.

Zubery Mwombeji.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba  8 mwaka huu majira ya saa  3:45 asubuhi, katika eneo la kitongoji cha Mabanda barabara ya kutoka Mateteleka kwenda Maweso katika kijiji cha Lilondo kata ya Wino wilayani humo.

Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo mwendesha bodaboda huyo akiwa anaendesha pikipiki yake aina ya SANLG ambayo namba zake za usajili hazikupatikana, alimgonga mwanafunzi huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lilondo na kumsababishia apoteze maisha yake.

Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kumgonga Martha alikimbia na kutokomea kusikojulikana ambapo Polisi kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kumsaka na mara tu atakapopatikana atafikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo linalomkabili.

Kamanda Mwombeji alifafanua kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi aliokuwa nao mwendesha bodaboda huyo, ambapo alishindwa kumudu usukani wa pikipiki yake na kupelekea kumgonga mtembea kwa miguu ambaye alikuwa kandokando mwa barabara hiyo.


Wakati huo Jeshi hilo la Polisi mkoani hapa, linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kukutwa na miche 270 ya bangi ambayo ilikuwa kwenye shamba lenye ukubwa wa robo heka katika kijiji cha Namasakata wilayani Tunduru.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, zubery Mwombeji amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Abbas Abbas (45) mkazi wa kijiji cha Chemchem, Fakih Rashid (19) mkazi wa kijiji cha Ligoma, Ally Juma (50) mkazi wa Tuwemacho, Mohamed Maloso (45) mkazi wa kijiji cha Chemchem na Omary Kalambo (26) mkazi wa Majengo Tunduru mjini.

Alifafanua kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wamepanda miche 270 ya bangi, kwenye shamba la ukubwa huo na mmoja kati yao ambaye ni Omary Kalambo alikutwa na kete moja ya bangi akiwa nayo mfukoni.


Hata hivyo alisema taarifa hizo zililizifikia Jeshi la Polisi kutoka kwa raia wema kwamba kuna kundi la watu ambao wanashirikiana kwa pamoja kulima shamba la bangi na Polisi baada ya kupata taarifa hizo, walianza kufuatilia  na kubaini ukweli uliopo kisha kuwakamata ambapo watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

No comments: