Tuesday, September 20, 2016

MANISPAA SONGEA YATUMIA MILIONI 448 UJENZI MRADI WA MAJI RUHUWIKO

Na Muhidin Amri,            
Songea.

MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma, inatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 448 kwa ajili ya kufanya kazi ya ujenzi wa mradi wa maji katika mtaa wa Ruhuwiko kanisani ili kuweza kuwaondolea kero wananchi ya ukosefu wa maji, ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa.

Samwel Sanya ambaye ni Mhandisi wa maji katika Manispaa hiyo, alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa tayari wamekwisha ingia mkataba na mkandarasi wa Kampuni ya Giraf Investment, kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi huo.

Alifafanua kuwa upembuzi yakinifu kwa mradi huo, umefikia asilimia 95 ambapo ulifanywa mwaka wa fedha wa 2012/2013 na kwamba ujenzi wake hivi sasa ambao unaendelea kutekelezwa, umefadhiliwa na benki ya dunia.


Sanya alieleza kuwa mkandarasi huyo hadi sasa amelipwa zaidi ya shilingi milioni 307 na kiasi ambacho bado anaidai Manispaa hiyo, ni zaidi ya shilingi milioni 181 hivyo atamaliziwa kulipwa mara baada ya kazi husika kukamilika kwake.

“Mradi huu bado haujakabidhiwa kwa wananchi, bado mkandarasi anatudai tunachosubiri hapa ni kukamilisha malipo ya mkandarasi huyu ili tuweze kuwakabidhi wananchi hawa”, alisema.

Alibainisha kuwa mradi huo unatumia nguvu ya umeme kupandisha maji kwenye tanki kubwa lililojengwa, hivyo watumiaji wa maji watatakiwa hapo baadaye kuchangia gharama kidogo ambazo zitasaidia kufanyia ukarabati pale patakapokuwa na hitilafu za kawaida.

Mbali na hilo lengo la idara hiyo pia ni kuukabidhi mradi huo, kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) ambao ndiyo watasimamia uendeshaji wake ili uweze kuwa endelevu.

Wakati huo huo Manispaa ya Songea, imekamilisha pia ukarabati wa visima viwili vya maji ambavyo vinatarajia kuhudumia watu zaidi ya 500.


Mhandisi Sanya amevitaja visima hivyo kuwa ni kile kilichopo katika shule ya sekondari Mdandamo kata ya Mletele mjini hapa, ambacho kimegharimu shilingi milioni 2.2 na kisima kingine cha shule  ya msingi Luhira kata ya Mshangano ambacho kimegharimu shilingi milioni 2.8.

No comments: