Sunday, October 2, 2016

WAJASIRIAMALI SONGEA WANUFAIKA NA MIKOPO YA BARAZA LA TAIFA



Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

BARAZA la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kushirikiana na benki ya Posta hapa nchini, limetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 542.8 kwa vikundi mbalimbali vya ujasiriamali wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Katibu mtendaji wa baraza hilo, Beng’i Issa alisema kuwa vikundi 28 ndivyo ambavyo vimepewa mkopo huo chini ya mwamvuli wa Masista wa shirika la DMI lililopo mjini hapa.

Issa alifafanua kuwa kati ya vikundi hivyo, saba vimeanzisha SACCOS ya Vijana na wengine ambao wapo Maposeni katika jimbo la Peramiho wilayani humo nao waliwezeshwa mikopo hiyo kwa ajili ya kufanyia shughuli zao za kimaendeleo.


Alisema kuwa vikundi hivyo pia awali vilipata mikopo yenye masharti nafuu kutoka katika benki hiyo kwa makubaliano maalumu na baraza hilo la taifa ambapo jumla ya wajasiriamali 711 waliweza kunufaika.

Vilevile kwa ufupi alibainisha kuwa wajasiriamali kutoka kikundi cha DMI Women group wamepata shilingi milioni 389.2, Maposeni SACCOS ilipewa shilingi milioni 132.2, Vikoba milioni 21.2, Vijana SACCOS nayo ilipewa shilingi milioni 100 ambapo kati ya wanafuika wa mikopo hiyo wanawake walikuwa 522 na wanaume 186.

Katibu huyo aliendelea kueleza kuwa kutolewa kwa mikopo hiyo ni utekelezaji wa makubaliano kati ya baraza hilo na benki ya Posta hapa nchini, ambayo yalisainiwa mapema mwezi Julai mwaka jana.

Alisema kuwa wadau mbalimbali wa maendeleo wameipongeza pia benki hiyo kwa kukubali kushirikana na baraza hilo katika kutekeleza makubaliano hayo kwa lengo la kuwasaidia Watanzania, hususani wajasiriamali wadogo kuweza kupata mikopo hiyo yenye lengo la kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo alisema kuwa asilimia 73 ya mikopo hiyo imeelekezwa zaidi kwa makundi ya wanawake ambao ndiyo nguzo ya familia kwani baraza linaamini kwamba, ukimwezesha mwanamke ni sawa na kuiwezesha familia nzima kwa sababu wanawake ndiyo wanaobeba majukumu mazito ya kutunza familia na jamii kwa ujumla.

No comments: