Saturday, October 29, 2016

MVUTANO HUU WA STENDI NI AIBU KWA VIONGOZI WA SERIKALI SONGEA



Na Kassian Nyandindi,           
Songea.

MVUTANO uliodumu kwa muda mrefu baina ya Wadau wa usafirishaji abiria pamoja na baadhi ya viongozi wa kisiasa na serikali ya mkoa wa Ruvuma, ambao ulihusisha matumizi ya vituo viwili vikubwa vya mabasi ya abiria mjini Songea umeelezwa kumalizika, baada ya kufanyika mazungumzo na kuwepo kwa makubaliabo ya pamoja kwa pande zote husika.

Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika Kituo cha mabasi mjini hapa,  ambao ulishirikisha baadhi ya Wadau hao, abiria na wananchi, Mstahiki  Meya wa Manispaa ya Songea Abdul Mshaweji pamoja na Mbunge wa jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama alisema kwamba baada ya mazungumzo yaliyochukua muda mrefu na kuibuka kwa msuguano juu ya matumizi ya vituo vikubwa viwili, yamemalizika kwa makubaliano yaliyoridhiwa na viongozi watano wa ngazi za juu katika mkoa na halmashauri hiyo ya Manispaa.

Mshaweji alisema kuwa vikao hivyo vilimhusisha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge, Katibu tawala wa mkoa huo Hassan Bendeyeko, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Songea Tina Sekambo, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Abdul Mshaweji na Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama ambapo pamoja wamekubaliana kuwa vituo vyote viwili vya mabasi ya abiria vitumike ambavyo ni kile kituo kilichopo mjini kati na cha Msamala.


Alifafanua kuwa uamuzi huo ambao ndiyo unasimamiwa na halmashauri hiyo ya Manispaa, uliamuriwa kwenye vikao halali vya baraza la madiwani wakati walipopata mkopo kutoka benki ya dunia kwa ajili ya kufanyika ukarabati wa kituo kikuu cha mabasi cha mjini kati, na kuanzishwa kwa kituo cha muda cha Msamala ili kupisha ukarabati huo uweze kufanyika.

Pia aliwaomba radhi wananchi kwa kuwepo kwa mvutano huo uliowaweka njia panda kwa muda mrefu kati ya wananchi wa Manispaa hiyo na nje ya manispaa, kushindwa kuelewa hatima ya uwekezaji wao walioufanya kwenye vituo vyote viwili.

Kwa ujumla mazungumzo hayo na makubaliano ya pamoja yalipofanyika na kuafikiana kuwa vituo vyote viwili vya mabasi vitumike kwa mabasi yanayotoka nje ya mkoa kuanzia safari zake, kwenye kituo cha mjini kati na kupitia kituo cha Msamala na kuendelea na safari huku yale yanayoingia kuanzia kituo cha Msamala na kumalizia safari zake kwenye kituo cha hapa mjini.

Naye Mbunge wa jimbo hilo Leonidas Gama alisema kuwa maamuzi hayo yana baraka zote kwa sababu yamefanyika kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma, pamoja na wageni wanaoingia na kutoka kwenye mkoa huo hivyo hakuna mshindi katika maamuzi hayo bali maslahi ya makundi yote ya wananchi ndiyo yaliyozingatiwa zaidi.

Hata hivyo pamoja na viongozi hao kutoa tamko hilo la kuruhusu kituo hicho cha mjini ambacho siku za karibuni kilianza kutumika kwa ajili ya daladala, kianze kutumiwa na mabasi makubwa ya abiria yanayoenda nje ya mkoa jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, limeendelea kuyazuia mabasi hayo kuingia kwenye kituo hicho kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria kwa kile kilichoelezwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Zubery Mwombeji kwamba Jeshi hilo linasimamia maamuzi yalitotolewa awali na halina taarifa ya mabadiliko hayo.

No comments: