Saturday, October 22, 2016

MBINGA WAANZA KUTEKELEZA ZOEZI LA UPIMAJI ARDHI



Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imeanza kutekeleza mpango wake wa zoezi la upimaji ardhi katika maeneo ambayo yana rasilimali muhimu za kudumu kama vile mashamba ya kahawa na miti, ili kuweza kuyaongezea thamani na kuwafanya wakulima waweze kupata mikopo katika taasisi za kifedha na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.

Aidha imeelezwa kuwa mpango huo unalenga kupima ekari zaidi ya 68,000 na kwamba mpaka sasa tangu zoezi hilo lianze tayari ekari 12,600 zimepimwa na kwamba kazi hiyo imefanyika katika kipindi cha wiki moja.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Gombo Samandito alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ambao walitembelea katika baadhi ya vijiji, ambavyo zoezi hilo la upimaji linaendelea kufanyika.


Samandito alisema kuwa zoezi hilo linaenda sambamba na upimaji wa miji midogo ambapo katika wilaya ya Mbinga tayari miji yake mitano ya Kigonsera, Ruanda, Matiri, Mkako na Kiamili kazi inaendelea ya uchukuaji wa takwimu za awali katika maeneo yenye nyumba na viwanja.

“Kazi za kiutendaji zaidi wa kiofisi ikiwemo uaandaji wa ramani za msingi (Base map) unaendelea kufanyika, tuna makampuni matano ambayo yanafanya kazi hii ya upimaji”, alisema Samandito.

Alifafanua kuwa hapo baadaye baada ya kukamilisha zoezi la upimaji mashamba yenye mazao hayo ya kudumu kama vile kahawa na miti, pia watapima kwenye mashamba ambayo yana mazao ya muda ikiwemo mahindi na mengineyo.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa mpaka sasa kati ya kata 29 zilizopo wilayani humo tayari kata 20 zimeanishwa kwa ajili ya zoezi hilo la upimaji wa ardhi ya wananchi wake ili waweze kupata hati miliki za kimila ambazo ni kata ya Kipapa, Langiro, Maguu, Mapera, Kambarage, Mikalanga, Nyoni, Mpapa, Mbuji, Litembo, Kitura, Ngima, Wukiro, Kipololo, Ukata, Linda, Mkumbi, Kihangimahuka, Lukarasi na Matiri.

No comments: