Tuesday, October 4, 2016

HURUMA WATOA MSAADA WA NGUO KWA WATOTO YATIMA NAMTUMBO

Na Yeremias Ngerangera,        
Namtumbo.

MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Luckness Amlima ameipongeza asasi isiyokuwa ya serikali ya Huruma iliyopo wilayani hapa kwa kutoa msaada wa nguo kwa watoto yatima 308 ambao wanaishi katika mazingira magumu, ambazo hutoka katika kata ya Rwinga na Namtumbo mjini hapa.

Pongezi hizo alizitoa wakati alipokuwa akizungumza juzi na wananchi mjini Namtumbo, wakati wa zoezi la ugawaji wa nguo hizo za watoto hao zilizotolewa na Shirika la Japan Relief Center (JRC) kutoka nchini Japan kupitia asasi hiyo.

Amlima alisema kuwa kuna kila sababu kwa asasi nyingine zilizopo ndani na nje ya wilaya hiyo, kuiga mfano kama huo wa kusaidia watoto hao kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali muhimu ili waweze kuondokana na dhana ya kujisikia kama vile wametengwa.


Naye Mkurugenzi wa asasi ya Huruma, Asumpta Ndauka aliwataka wazazi wilayani Namtumbo kuwalea watoto hao kikamilifu na kuacha tabia ya kuwatenga au kuwanyanyasa kwa namna moja au nyingine.

Kwa upande wake mtoto Ashura Mohamed (10) aliushukuru uongozi wa asasi hiyo kwa kuwaletea nguo hizo ambapo alisema kuwa, zitaweza kuwafanya waweze kuvaa na kupendeza kama walivyo watoto wengine.


Shirika la Huruma ni asasi isiyokuwa ya serikali ambayo hujishughulisha na kuhudumia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu, wajane, kutoa elimu juu ya kuepukana na maambukizi ya Virusi  vya ukimwi na utunzaji  wa  mazingira.

No comments: