Friday, October 7, 2016

DOKTA MAHENGE ASIKITISHWA NA ONGEZEKO LA MIMBA ZA WANAFUNZI WA KIKE MBINGA

Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amesikitishwa na idadi ya ongezeko la mimba kwa watoto wa kike wanaosoma shule za sekondari wilayani Mbinga mkoani humo, jambo ambalo linasababisha washindwe kuendelea na masomo yao.

Dkt. Binilith Mahenge.
Jumla ya wanafunzi wa kike 37 wanaosoma katika shule za sekondari zilizopo katika maeneo mbalimbali wilayani humo wamepewa ujauzito na kesi zao zimefikishwa Polisi, ili watuhumiwa waliohusika na vitendo vya kukatisha masomo ya watoto hao waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Dkt. Mahenge alipokea taarifa ya kesi hizo ambayo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye juzi alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa, ambapo Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mimba hizo wamepewa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu.

Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa mkoa ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha kwamba, suala hilo linatekelezwa kikamilifu kwa kuhakikisha watuhumiwa wote waliohusika kufanya vitendo hivyo wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.


“Mnasema uchunguzi bado unaendelea, natoa agizo kwenu viongozi wote wa wilaya hii hakikisheni jambo hili linafanyiwa kazi haraka na kwa wakati wahusika wa vitendo hivi, wanakamatwa haraka na kufikishwa kwenye mkono wa sheria”, alisisitiza Dkt. Mahenge.

Awali Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alimweleza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge kuwa kesi hizo za kuwapatia ujauzito watoto hao wa shule za sekondari zimekwama Polisi na bado hazijafikishwa mahakamani kutokana na jamii kutotoa ushirikiano wa karibu wakati wa kuwakamata watuhumiwa waliohusika na vitendo hivyo.

"Kwa upande wa shule za msingi tatizo hili hapa wilayani hakuna, limekuwa likitusumbua hasa kwa shule za sekondari, wazazi wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha katika kukabiliana nalo", alisema Nshenye.


Nshenye aliongeza kuwa uchunguzi juu ya tatizo hilo bado unaendelea ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa na kuweza kupunguza tatizo hilo, ambalo linakatisha ndoto za maendeleo ya watoto wa kike katika nyanja ya elimu.

No comments: