Sunday, October 30, 2016

TUNDURU YATENGA MAENEO YA KUENDESHA KESI ZA WANAUME WANAOWAPA MIMBA WANAFUNZI WA KIKE

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera akipata chakula cha mchana na baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Mataka iliyopo wilayani humo.


Na Muhidin Amri,               
Tunduru.

WILAYA ya Tunduru imetenga maeneo maalum wilayani humo, kwa ajili ya kuendesha na kusikiliza kesi na mashauri mbalimbali yanayohusu Wanaume wanaowapa mimba watoto wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa wilaya  hiyo, Juma Homera wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi pamoja na wazazi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Masonya, katika mahafali ya  11 ya kidato cha nne kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Homera alieleza kuwa imebainika kuwa kushuka kwa ufaulu wa mitihani kwa wasichana wengi katika shule za sekondari wilayani humo, kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na wanafunzi wa kike kujihusisha na mambo ya kimapenzi hivyo kuwafanya kutozingatia masomo yao ipasavyo.


Alisema kuwa ili kukomesha tatizo hilo ameiagiza idara ya Mahakama kuendesha kesi za watu wanaotuhumiwa kuwapa mimba wanafunzi hao, zifanyike huko huko katani kwa mfumo wa Mobile court, ili kuharakisha usikilizaji wa kesi hizo kwa kuwarahisishia hata mashahidi kutokwenda mbali wakati wa kutoa ushahidi wa mashauri hayo.

Sambamba na kuwafikisha Mahakamani wanaume wanaosababisha mimba hizo Mkuu huyo wa wilaya, amewaonya wazazi wa watoto ambao watapata mimba na kufanya makubaliano ya kumalizana kimya kimya, endapo watabainika kufanya hivyo nao washtakiwe ili iweze kuwa fundisho kwa wengine.

“Kuanzia sasa Mahakimu watazunguka kila kata kushughulikia kesi za mimba za wanafunzi ili kumaliza kabisa tatizo hili la mimba, kwa wanafunzi wa kike hapa wilayani”, alisema.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru, Homera aliwapongeza walimu wa shule ya sekondari Masonya kwa kutoa elimu kiwango cha juu na kuifanya shule hiyo kuongoza kimkoa na kuwa moja ya shule bora 100 Kitaifa kwa mitihani ya kidato cha sita mwaka jana, huku akiwataka wanafunzi wa kidato cha nne mwaka huu nao kuvunja rekodi ya ufaulu.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkuu wa shule hiyo Elice Banda aliwataka wazazi kuwapatia watoto wao mahitaji yote muhimu ili kuepuka kushawishika kupokea misaada kutoka kwa mafataki wanaowapatia mimba watoto hao.

Banda alimweleza Mkuu huyo wa wilaya kwamba, shule  yake ina wanafunzi wa kike 533 wa kidato cha kwanza hadi cha sita na kwamba inakabiliwa na msongamano wa sehemu ya malazi kutokana na mabweni yaliyopo kutokidhi mahitaji husika.

No comments: