Sunday, October 2, 2016

FIGISU FIGISU ZAWATESA CHADEMA SONGEA WANACHAMA WAVULIWA MADARAKA



Na Kassian Nyandindi,        
Songea.

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, kimewavua madaraka wanachama wake sita na wajumbe watano wa Kamati tendaji ya chama hicho wilayani humo kwa muda wa miezi 30.

Imefafanuliwa kuwa kuvuliwa madaraka kwa wanachama na wajumbe hao, kumetokana na kudaiwa kwamba walikihujumu chama hicho wakati wa uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana na kusababisha mgombea Ubunge kupitia tiketi ya CHADEMA Jimbo la Songea mjini, Joseph Fuime kushindwa kupita katika chaguzi hizo.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti CHADEMA Taifa.
Akizungumza waandishi wa habari mjini hapa, Katibu wa Chama cha demokrasia na maendeleo mkoa wa Ruvuma, Delphin Gazia alisema kuwa wanachama hao wamevuliwa uanachama tangu Septemba 14 mwaka huu kutokana na sababu hizo.

Gazia aliwataja wanachama hao waliofutwa kwenye daftari la orodha ya wanachama kuwa ni Rhoda Komba aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) wilayani songea, ambaye pia katika kipindi kilichopita alikuwa ni diwani wa viti maalum toka kata ya Mfaranyaki Manispaa ya Songea na Seiph Ahmed Seiph ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la wazee la wilaya hiyo.


Wengine ni Omary Hassan ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA) wilayani humo, Ajaba Nditti na Swedi Millanzi ambao walikuwa ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya wilaya na Emmanuel Kalisinje ambaye alikuwa mjumbe kamati ya utendaji ambapo alivuliwa uanachama huo, akidaiwa kutenda kosa la kuiba nyaraka muhimu za chama na kuzipeleka  kwa makada wa vyama vingine vya siasa. 

Alisema kuwa wanachama hao waliovuliwa uanachama kuanzia ssa hawataruhusiwa  kufanya shughuli ya aina yoyote ya chadema kwani imebainika kuwa ndio waliokihujumu chama kwenye kipindi cha kampeni hadi siku ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi.

Katibu huyo wa CHADEMA alieleza kuwa wakati wa kipindi cha kampeni chaguzi zilizopita, kiliunda tume maalumu ambayo ilipewa jukumu la kuratibu shughuli mbalimbali za uchaguzi mkuu, lakini timu hiyo cha kushangaza badala ya kusimamia shughuli za chama iliamua kufanya tofauti na wakati wote ikitoa siri za chama hicho kwa vyama vingine vya siasa jambo ambalo lilisababisha mgombea ubunge kupitia chama hicho jimbo la Songea mjini kushindwa.

Gazia alisema kuwa inaonesha wazi kuwa kulikuwa na figisu figisu walizozifanya ambazo zilitoa nafasi kwa mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangazwa kuwa ndiye aliyekuwa mshindi kwenye uchaguzi huo, kwani mgombea ubunge  wa CHADEMA baadaye ilibainika kuwa ndiye aliyepata kura nyingi tofauti na tangazo  lililotolewa na Mkurugenzi wa uchaguzi wa jimbo la Songea mjini, Raphael Kimari.

Alifafanua kuwa mgombe ubunge kupitia CHADEMA Fuime alipata kura 40,766 na jumla ya wapiga kura walikuwa 77,554 lakini  wakati wa  kutangazwa matokeo  takwimu hizo hazikutajwa  na mgombea alipotakiwa apeleke nakala za matokeo ya uchaguzi huo, alikataa jambo ambalo linaonesha kuwa kulikuwa na mchezo mchafu uliofanyika.

Wengine waliosimamishwa uanachama kwa muda wa miezi 30 kwa makosa ya utovu wa nidhamu wakituhumiwa kupita kila kata za chama hicho kuwashawishi vijana kufunga ofisi za CHADEMA na kupanga njama za mapinduzi kwa viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya Songea, kuwa ni  Sikitu Sallum ambaye alikuwa Katibu wa BAVICHA wa wilaya hiyo na Zuberi Tindwa ambaye alikuwa ni mhamasishaji ndani ya chama hicho.

Katibu huyo wa Chama cha demokrasia na maendeleo mkoa wa Ruvuma, Gazia alifafanua kuwa pamoja na viongozi hao kuwavua uanachama bado kamati ya utendaji ya mkoa inaendelea kufuatilia mwenendo wa Kampeni za uchaguzi Mkuu uliopita ili kuweza kuchukua hatua zaidi kwa aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Songea mjini kupitia tiketi ya chama hicho, Fuime ambaye alisimamishwa miezi kadhaa iliyopita baada ya kukaidi kuleta nakala halisi za matokeo ya uchaguzi huo mwaka jana.

No comments: