Friday, October 21, 2016

TFS MBINGA YATOA MSAADA WA MADAWATI KWA SHULE ZA MSINGI

Katibu tawala wilaya ya Mbinga, Gilbert Simiya wa pili kutoka kushoto akikata utepe ikiwa ni ishara ya tendo la kukabidhi madawati yaliyofadhiliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani hapa. (Picha na Muhidin Amri) 
Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

WADAU wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kuendelea kuchangia katika sekta ya elimu wilayani humo ili watoto wanapokuwa shuleni waweze kusoma wakiwa katika mazingira mazuri na kufanya vyema katika masomo yao.

Aidha taasisi mbalimbali nazo zimetakiwa kuhamasika kuchangia madawati shuleni na sio kuiachia serikali peke yake, kwani sekta ya elimu ili iweze kusonga mbele inahitaji mchango kutoka kwa wadau mbalimbali.


Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Gilbert Simiya alisema hayo juzi mjini hapa alipokuwa katika zoezi la kukabidhi madawati 80 kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo, ambayo yalitolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ikiwa ni mchango wa madawati hayo uliotolewa kwa ajili ya matumizi ya watoto wa shule za msingi wilayani hapa.

Simiya alikuwa akimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye ambapo alitoa pongezi kwa Wakala huyo kwa kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kutoa mchango huo wa madawati ili kusaidia kuboresha sekta hiyo ya elimu.


“Mchango huu utasaidia watoto wetu kukaa katika mazingira mazuri ya kusomea natoa pongezi kwa watumishi wa TFS kwa kufanya jitihada ya kutengeneza madawati haya, natoa wito kwa taasisi zingine nazo zihamasike kuchangia katika sekta hii ya elimu hapa Mbinga”, alisema.

Awali akitoa taarifa ya Wakala wa huduma za misitu Tanzania, Meneja wa TFS wilayani Mbinga Festo Chaula alisema kuwa wametoa mchango wa madawati hayo kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata mafunzo katika mazingira mazuri shuleni.

Pia Chaula alifafanua kuwa dira yao ni kuwa taasisi bora katika uhifadhi wa rasilimali misitu na nyuki ikiwemo na upatikanaji bora na endelevu wa mazao yatokanayo na misitu kwa kuhakikisha kunakuwa na usimamizi endelevu ili zichangie mahitaji ya kijamii, kiuchumi, kiikolojia na kiutamaduni kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Alisema kuwa mojawapo ya malengo ya mpango mkakati wa TFS ni kuboresha rasilimali hizo na mfumo wa ikolojia (Forest and bee resource base and ecosystem improved) ambapo kuna dhima ya uwezeshaji jamii kwa kutoa ushiriki mpana wa wananchi katika kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa na kutumiwa kwa manufaa ya jamii.

Pamoja na mambo mengine kwa upande wake Ofisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Samwel Komba alitoa shukrani kwa msaada wa madawati waliyoyapata kutoka kwa Wakala huyo wa misitu Tanzania, huku akieleza kuwa yataweza kusaidia kukalia watoto 240 watakao kuwa darasani wakati wa masomo.


Hata hivyo wilaya ya Mbinga hivi sasa haina upungufu wa madawati ya kukalia wanafunzi shuleni ambapo imeweza kuvuka lengo kwa kutengeneza madawati 19,572 huku mahitaji halisi yakiwa ni madawati 19,421.

No comments: