Monday, October 31, 2016

WENYEVITI NA WATENDAJI WA VIJIJI MBINGA WANYOSHEWA KIDOLE KWA KUTOSOMA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA WANANCHI



Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

WENYEVITI na Watendaji wa vijiji na kata katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamenyoshewa kidole na kuelezwa kuwa katika maeneo yao ya kazi wamekuwa hawasomi taarifa za mapato na matumizi na kuwafanya wananchi walalamikie hali hiyo, huku baadhi ya maeneo wengine wakigomea hata kushiriki katika kufanya shughuli za maendeleo.

Aidha imefafanuliwa kuwa kutokana na tatizo hilo kuendelea kushamiri na kuwa kero katika jamii, kuna kila sababu sasa kwa uongozi wa halmashauri hiyo kupitia kitengo chake cha ukaguzi wa ndani kumpeleka mkaguzi huyo ili aweze kufanya ukaguzi katika vijiji na kata zote, ambazo kuna taarifa zenye utata juu ya mapato na matumizi ya fedha za wananchi.

Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo walilalamikia hali hiyo juzi kwa nyakati tofauti, katika kikao chao cha baraza la madiwani kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Vivian Mndolwa alisema kuwa tayari hatua za ukaguzi zimeanza kuchukuliwa katika baadhi ya vijiji na kata ambazo zimeonesha kuwa na matatizo hayo, huku akisema kazi hiyo imekwisha fanyika katika vijiji vya Ntunduaro, Myao na kata ya Ruanda.

Mndolwa aliongeza kuwa kutokana na uwepo wa uhaba wa rasilimali fedha na watumishi katika idara ya ukaguzi, wamekuwa wakiendelea na ukaguzi kwa awamu na taarifa zitaendelea kutolewa kwa kila kaguzi inapofanyika kupitia vikao husika.

“Pale Diwani anapogundua kwamba kuna tatizo ni vizuri atoe taarifa mapema katika ofisi ya Mkurugenzi, ili ofisi yetu ya ukaguzi iweze kuchukua hatua haraka na kumaliza migogoro iliyopo huko’, alisisitiza Mndolwa.

No comments: