Tuesday, October 25, 2016

WANANCHI RUVUMA WALALAMIKIA WABUNGE WAO

Na Julius Konala,       
Songea.

BAADHI ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma wamewalalamikia Wabunge wa mkoa huo, kwa kushindwa kuwa na umoja katika kupigania suala la shirika la ndege za serikali (ATC) kutua kwenye uwanja wa Manispaa ya Songea mkoani humo, wakidai kuwa ni muda mrefu sasa umepita mkoa huo umesahaulika katika masuala ya usafiri wa anga.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na wananchi hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Songea, ambapo wamedai kuwa wanashindwa kusafiri mara kwa mara kwa ndege ya Kampuni ya mtu binafsi inayofanya safari zake jijini Dar es salaam hadi Songea kutokana na gharama zake kuwa kubwa.

Mmoja wa wakazi wa Manispaa hiyo, Mohamed Abdallah alisema kuwa wananchi wa mkoa huo wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wa kusafiri kwa basi hadi mkoa wa Mbeya, kwa ajili ya kufuata huduma ya usafiri wa anga wakati usafiri huo endapo ungefanya safari zake mkoani humo na kwa bei ndogo ungesaidia kwa kiasi kikubwa hata kuleta wawekezaji na watalii watakaotembelea fukwe za ziwa Nyasa na wananchi kusafiri kwa ndege hizo.


“Mategemeo ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma ni kwamba wabunge wetu wangeweza kupigania ndege hizi zifanye safari zake hadi mkoani hapa, kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wa kusafiri kwa gharama kubwa wananchi wao badala ya kushughulika kila mmoja na jambo la jimboni kwake”, alisema Abdallah.

Alisema kuwa mkoa huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa umeme wa uhakika, jambo ambalo linapaswa kupiganiwa na wabunge hao katika kuonesha juhudi ya kuharakaisha umeme wa Gridi ya taifa unaingia mkoani humo badala ya kuona suala hilo kama ni la mtu mmoja.

Naye Colletha Ndunguru mkazi wa wilaya ya Mbinga mkoani hapa, alisema kuwa endapo wabunge hao hawataungana kwa pamoja katika kupigania maendeleo ya mkoa huo kwa pamoja kama ilivyokuwa kwa wabunge wengine wanaotokea mikoa ya Kaskazini, ndoto za Rais wa serikali ya awamu ya tano Dokta John Magufuli ya kuwa na Tanzania yenye viwanda itakuwa ni ndoto kwa mkoa wa Ruvuma badala yake wananchi wake watakuwa mashuhuda wa kushuhudia mikoa mingine itakavyopiga hatua mbele kimaendeleo.

Vilevile Angela Komba mkazi wa wilaya ya Namtumbo naye alisema kuwa wananchi wa mkoa huo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo inabidi zitatuliwe na wabunge wao ikiwemo kutafuta masoko ya kuuzia mazao yao, kupigania fidia za wananchi waliochukuliwa maeneo yao, kupigania ujenzi wa miundombinu ya barabara za makao makuu ya wilaya kwa kiwango cha lami pamoja na kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya maji vijijini na mjini, badala ya kuendeleza malumbano na migogoro isiyokuwa ya lazima.

No comments: