Sunday, October 30, 2016

KANISA LA AGAPE SONGEA LASIKITISHWA WAUMINI WAKE KUYUMBISHWA



Na Muhidin Amri,           
Songea.

WAUMINI wa Kanisa la AGAPE hapa mkoani Ruvuma, wametakiwa kutoyumbishwa na Waumini wa madhehebu mengine kwa lengo la kuhama Kanisa hilo, kwani imeelezwa kuwa endapo watafanya hivyo ni sawa na kuisaliti imani yao.

Askofu wa Kanisa hilo mkoani hapa, Asangalwisye Mwangakala alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa mara baada ya ibada ya kuwasimika Wachungaji 17 watakaofanya kazi ya kueneza injili katika maeneo mbalimbali mkoani humo.

Mwangakala alisema kuwa, hivi sasa kumekuwa na tabia kwa baadhi ya waumini wa madhehebu mengine kuwarubini waumini wake ili waweze kulihama Kanisa hilo, jambo ambalo likiendelea kufanyika linaweza kuleta chuki miongoni mwa Wakristo mkoani hapa.


“Ninawaomba waumini wangu wasikubali kutanga tanga kutokana na tamaa ya ushawishi fulani, bali yatupasa tuwe imara katika imani ya kanisa letu na tusikubali kuyumbishwa na madhehebu mengine”, alisema.

Kwa mujibu wa Askofu huyo aliongeza kuwa baadhi ya waumini wa madhehebu mengine wamekuwa na tabia ya kushawishi waumini wa kanisa lake wajiondoe na kwenda kwao, kwa lengo la kutaka kuwavuruga hivyo wanatakiwa kuendelea kuwa imara na kudumu katika imani yao.

Aliwataka waumini hao pamoja na wachungaji wapya, wakati wote kuhakikisha kwamba wanadumisha umoja, amani na upendo miongoni mwao na kujitokeza kushiriki kazi mbalimbali za kijamii katika misiba na hata kushiriki katika ujenzi wa shughuli za kimaendeleo.

Pia amewataka kushiriki na kuhamasisha jamii juu ya suala la kupeleka watoto wao shule, ili waweze kupata elimu na kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe kazini na kuwafichua watumishi wa umma wanaoendelea kufanya kazi kwa mazoea ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwa manufaa ya umma.

No comments: