Tuesday, October 4, 2016

AKUTWA CHUMBANI AKIWA AMEJINYONGA KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI

Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

MKAZI mmoja wa mtaa wa Furaha stoo Mbinga mjini, Digna Chikuli (22) amefariki dunia baada ya kukutwa amejinyonga na mwili wake ukiwa unaning’inia chumbani kwake, katika kenchi za nyumba aliyokuwa akiishi.
Zubery Mwombeji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 30 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi.

Mwombeji alifafanua kuwa chanzo cha tukio hilo kilisababishwa na wivu wa kimapenzi, baada ya marehemu huyo kumfumania hawara yake akiwa na mpenzi mwingine.

Alisema kuwa taarifa za kumfumania hawara yake, zilitolewa na majirani wenzake wanaoishi katika mtaa huo na kwamba marehemu Digna alipotoweka katika eneo la fumanizi, ndipo baadaye walipata taarifa kuwa amejinyonga.


“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Mbinga, ukisubiri ndugu wauchukue kwa ajili ya taratibu zingine za mazishi ili ziweze kuendelea kufanyika”, alisema.

Hata hivyo Kamanda Mwombeji alieleza kuwa jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, ili waweze kubaini ukweli na chanzo halisi juu ya tukio hilo.


No comments: