Monday, October 17, 2016

RC RUVUMA AKEMEA KITENDO CHA WATUMISHI WA SERIKALI MBINGA KUFANYABIASHARA YA MAGOMA YA KAHAWA

Na Kassian Nyandindi,             
Mbinga.

BAADHI ya Watumishi wa serikali waliopo katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamelalamikiwa wakidaiwa kutumia muda mwingi kufanya biashara haramu ya magoma ya kahawa licha ya serikali kukemea vitendo hivyo kwa muda mrefu ikiwataka waache mara moja.

Aidha wamenyoshewa kidole kwamba kwa kuwa ndiyo wamekuwa vinara namba moja kufanya biashara hiyo kwa lengo la kumdhulumu mkulima anayezalisha zao hilo, kwa atakayekamatwa atapewa adhabu kali ikiwemo kufikishwa mahakamani ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alimweleza hayo Mkuu wa mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge wakati alipokuwa amewasili wilayani hapa katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.


Nshenye alimweleza Dkt. Mahenge kuwa pamoja na serikali kupiga marufuku biashara hiyo bado kuna watumishi wachache wa umma, wamekuwa wakiendelea kuifanya na kwamba serikali imeweka mitego yake ili kuweza kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Tatizo kubwa hapa washiriki ni viongozi wenyewe wa serikali kutoka ndani ya halmashauri, nimetoa maagizo kwa kamati yangu ya ulinzi na usalama kushughulikia tatizo hili kwa nguvu zote”, alisema Nshenye.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge amemtaka Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga kusimamia ipasavyo sheria zilizopo juu ya namna ya kudhibiti biashara hiyo ya magoma ya kahawa ili mkulima asiweze kuibiwa kahawa yake.


Dkt. Mahenge alisisitiza kuwa kwa mtu yeyote atakayematwa awe ni mtumishi wa serikali au la, afilisiwe kahawa aliyokamatwa nayo na kupigwa faini sambamba na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kukiuka taratibu na sheria zilizowekwa na serikali.

No comments: