Sunday, October 23, 2016

WANANCHI KATA YA MKUMBI WAMLALAMIKIA DIWANI WAO WAUTAKA UONGOZI WA WILAYA KUINGILIA KATI KUMALIZA MGOGORO ULIOPO


Baadhi ya wananchi wa kata ya Mkumbi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakionesha kwa Waandishi wa habari jana (hawapo pichani) nyumba inayoendelea kujengwa na diwani wa kata ya Mkumbi Thomas Kapinga ambayo inadaiwa ipo ndani ya eneo lililotengwa kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha afya cha kata ya Mkumbi.

Wananchi wa kata ya Mkumbi wakiwa na vifaa mbalimbali kama vile magongo na matofali wakitaka kuvunja nyumba ya diwani wa kata hiyo, Thomas Kapinga kwa kile walichoeleza kuwa nyumba hiyo imejengwa katika eneo la zahanati ya kijiji cha Mkumbi ambayo inatumiwa na wananchi wote wa kata hiyo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za matibabu, hata hivyo diwani huyo amekataa kusimamisha ujenzi kwa madai kwamba eneo hilo ni la kwake. (Picha zote na Muhidin Amri)
Na Kassian Nyandindi,            
Mbinga.

BAADHI ya Wananchi wa kata ya Mkumbi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesema kwamba hawana imani na diwani wao wa kata hiyo, Thomas Kapinga kutokana na diwani huyo kudaiwa kuvamia eneo la kituo cha afya cha kata hiyo na kufanya shughuli za ujenzi wa nyumba yake binafsi.

Aidha walisema kuwa diwani huyo anafahamu kuwa eneo hilo lilitolewa na Wazee wa kata hiyo tokea miaka 1970 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo cha afya ikiwemo nyumba za kuishi watumishi, lakini wanamshangaa leo ameibuka na kudai kuwa ni la kwake na kuanza kufanya shughuli hizo za ujenzi.

Hayo yalisemwa na wananchi hao kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, ambao walitembelea katika kata hiyo kujionea maendeleo ya kituo cha afya kata ya Mkumbi.

Kufuatia hali hiyo wananchi hao wameutaka uongozi wa wilaya hiyo kuingilia kati na kuona namna ya kumaliza mgogoro huo, ambao sasa umedumu kwa muda mrefu bila kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.


Mwenyekiti wa baraza la Wazee kata ya Mkumbi, Gaufrid Mazungumzo alisema kuwa wao hivi sasa hawaoni sababu ya kuongozwa na diwani ambaye hapendi kusikiliza mawazo ya wananchi wake ya kimaendeleo, kwani wao walitoa eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja na nusu kwa ajili ya kupanua ujenzi huo wa kituo cha afya.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Mkumbi, Benuard Komba alifafanua kuwa kitendo cha diwani wao Kapinga kuonesha waziwazi vitendo vya kupingana na wananchi wake ni dhahiri ameshindwa kuongoza kata hiyo, hivyo wamemtaka ajiondoe mapema yeye mwenyewe katika nafasi hiyo kabla hawajachukua hatua ya kumtaka aachie ngazi.

“Ninataka kusema hivi katika eneo hili analogombea na wananchi sio la kwake, sisi wananchi ndiyo tulilitoa kwa ajili ya matumizi ya kijamii na sio kwa matumizi ya mtu binafsi, kwa ajumla serikali ya kijiji chetu haikubaliani na vurugu hizi za diwani huyu”, alisema Komba.

Vilevile Christopher Kongalipongo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Mkumbi aliongeza kuwa wanamshangaa diwani Kapinga waliyemchagua awaongoze kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye, amekuwa wa kwanza kupinga maendeleo ya wananchi wake na kutengeneza migogoro ya ardhi isiyokuwa na tija.

“Wazee wa kata hii ya Mkumbi tunaomba kilio chetu kimfikie Rais John Magufuli ambaye ndiye Mwenyekiti wetu wa Chama, achukue hatua dhidi ya diwani huyu ambaye anatunyanyasa tumechoka kuvumulia upuuzi huu”, alisema Kongalipongo.

Alipoulizwa diwani wa kata ya Mkumbi, Kapinga alikiri kuwepo kwa mgogoro huo kati yake na wananchi hao na kueleza kuwa eneo lenye mgogoro ni mali yake na yeye anawashangaa wananchi wa kata hiyo, wakisema kuwa lilitengwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kijamii.

Hata hivyo Kapinga alisema kuwa eneo hilo ni mali yake na ndugu zake, hivyo hawezi kuliacha likapotea kienyeji vinginevyo wamlipe fidia kwanza endapo kama kuna mtu analihitaji kufanyia shughuli yoyote ya kimaendeleo.

No comments: