Sunday, October 16, 2016

SEKONDARI YA WASICHANA MBINGA WAKABILIWA NA UPUNGUFU WA MABWENI YA KULALA WANAFUNZI

Na Kassian Nyandindi,             
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa tatizo la kulala wanafunzi wawili kitanda kimoja katika bweni la shule ya Sekondari wasichana Mbinga iliyopo mkoani Ruvuma, inatokana na upungufu mkubwa uliopo wa majengo na vyumba vya kulala watoto hao katika shule hiyo, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua za haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha kwamba unatenga fedha kupitia vyanzo vyake vya mapato ya ndani, kwa ajili ya kuweza kuanza taratibu za ujenzi wa bweni hilo la kulala watoto hao ili waweze kuondokana na adha hiyo wanayoipata sasa.

Dkt. Mahenge alitoa agizo hilo hivi karibuni alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoani hapa, kukagua maendeleo ya shule za sekondari kwa lengo pia la kujionea changamoto mbalimbali zilizopo kwenye shule hizo na kuzitafutia ufumbuzi wake.


“Nimegundua hapa kuna tatizo kubwa la upungufu wa vyumba vya kulala watoto hawa, nauagiza uongozi wa wilaya uone namna ya kutafuta fedha kupitia mapato yenu ya ndani ili kuweza kumaliza tatizo hili mapema la ujenzi wa bweni jipya la kulala hawa wanafunzi”, alisisitiza.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa alipozungumza na wanafunzi wa shule hiyo ambayo ni ya mchepuo wa masomo ya sayansi inayojumuisha watoto wa kike tu, aliwataka watoto hao kusoma kwa bidii ili serikali hapo baadaye iweze kuwapata wataalamu wa kutosha katika fani ya masomo hayo.

Alibainisha kuwa kitakachoweza kuwakomboa wananchi wa bara la Africa katika kuondokana na umaskini ni sisi wenyewe kuweka jitihada katika kuzingatia suala la elimu, kwa wazazi kupeleka watoto wao shule na kusoma kwa juhudi na maarifa ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo.

Kwa upande wake akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya shule ya sekondari ya wasichana Mbinga, Makamu mkuu wa shule hiyo Rehema Rohomoja alimweleza Dkt. Mahenge kuwa halmashauri ya wilaya Mbinga tayari imetenga fedha shilingi milioni 160.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya kulala watoto hao.


Rohomoja aliongeza kuwa ujenzi huo wa bweni jipya unatarajiwa kuanza mapema kuanzia sasa, baada ya taratibu za mchakato wa kumpata mkandarasi husika na mwenye sifa kukamilika kwake.

No comments: