Friday, October 7, 2016

KIWANDA CHA KUKOBOA KAHAWA MBINGA CHAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Kahawa iliyosindikwa yenye jina maarufu Mbinga Cafe ni sehemu ya bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

IMEBAINISHWA kuwa uzalishaji mdogo wa kahawa ya maganda katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na ongezeko la ushindani katika biashara ya ukoboaji wa kahawa ni changamoto kubwa inayokikabili Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Mbinga (MCCCO) kwani kimekuwa kikipokea zao hilo kiasi kidogo tofauti na uwezo mkubwa ilionao wa kukoboa kahawa.

Pamoja na Kiwanda hicho kujengwa kuwa na uwezo mkubwa wa kukoboa kahawa zaidi ya tani 30,000 kwa mwaka, bado uzalishaji wa za hilo wilayani humo umekuwa ni mdogo kutoka kwa wakulima ambapo kwa mwaka wamekuwa wakizalisha tani 5,000 hadi 17,500 tu hali ambayo imekuwa ikisababisha kushindwa kufikia malengo husika.

Aidha kwa upande wa ushindani wa biashara ya ukoboaji kahawa umeongezeka kutokana na mji wa Mbinga peke yake hivi sasa, kuna viwanda vitatu vya kukoboa zao hilo hivyo kutokana na uzalishaji kuwa kidogo kutoka kwa mkulima, kahawa inayozalishwa imekuwa ni ya mtindo wa kunyang’anyana.

Hayo yalisemwa na Meneja Mkuu wa kiwanda cha kukoboa kahawa wilayani Mbinga, Jonas Mbunda alipokuwa akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya kiwanda hicho kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge aliyetembelea juzi kujionea maendeleo mbalimbali kiwandani hapo.


“Mheshimiwa mkuu wa mkoa pamoja na changamoto hizi tulizonazo hapa wilayani, lakini sisi hapa kwetu kiwandani bado tunaongoza kupokea kahawa nyingi kutoka kwa mkulima mmoja mmoja na vyama vya ushirika”, alisema Mbunda.

Mbunda alisema kuwa katika msimu wa mwaka huu, MCCCO wanatarajia kukoboa zaidi ya tani 10,000 na kwamba katika kuongeza mapato ya kampuni hiyo wamekuwa wakitoa huduma nzuri ya ukoboaji na utunzaji kahawa kwa vyama vya ushirika, vikundi vya wakulima na wafanyabiashara wenye makampuni binafsi jambo ambalo huwafanya waweze kukoboa zaidi ya asilimia 60 ya kahawa inayozalishwa Mbinga.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge aliwataka wataalamu wa kilimo wa wilaya ya hiyo kwa kushirikiana na Menejimenti ya Kampuni hiyo ya kukoboa kahawa wilayani hapa, wajenge ushirikiano wa kuongeza mitambo midogo ya kuchakata kahawa mbivu vijijini ili kuweza kuongeza ubora wa zao hilo na kuwavutia wakulima wengi kuleta kahawa yao kukoboa katika kiwanda hicho.

Dkt. Mahenge alisisitiza kuwa lengo kubwa la serikali ni kuona inaboresha viwanda vyake kwa kuhakikisha kwamba vinafanya kazi iliyolengwa, ili kuweza kuinua uchumi wa mkulima mwenye kipato cha chini taifa kwa ujumla kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.


Hata hivyo Kampuni ya kukoboa kahawa Mbinga inamilikiwa kwa pamoja kati ya vyama vya ushirika 28 vinavyolima kahawa nchini Tanzania na serikali kwa ujumla, ambapo vyama vya ushirika vinamiliki asilimia 56.54 ya hisa zote na serikali asilimia 43.46 ambapo umiliki huo ulianza rasmi Septemba 18 mwaka 1995 wakati kampuni hiyo ilipoanza kubinafsishwa.

No comments: