Saturday, October 29, 2016

WAKAZI MATETEREKA MADABA WADAIWA KUWEKEWA SUMU KWENYE CHANZO CHA MAJI SERIKALI YAOMBWA KUINGILIA KATI

Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

WAKAZI waishio katika kijiji cha Matetereka katika kata ya Matetereka Jimbo la Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wameuomba uongozi wa mkoa huo kuingilia kati na kumchukulia hatua Mwenyekiti wa kijiji hicho, Remigius Njafula ambaye anatuhumiwa kuwalinda kwa kuwakumbatia baadhi ya wananchi wanaolalamikiwa kuweka sumu katika chanzo cha maji kinachotumiwa na wananchi hao.

Mkuu wa mkoa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge.
Aidha kufuatia tukio hilo wameuomba pia uongozi huo wa mkoa kuwasaidia kumwondoa madarakani Mwenyekiti huyo, kutokana na kitendo hicho cha kuwabeba watu wanaotuhumiwa kuweka sumu aina ya Round up ambayo inatumiwa kuulia magugu shambani.

Tukio hilo hivi sasa limesababisha kwenye chanzo hicho cha maji kijijini Matetereka, kaya zaidi ya 50 kukosa huduma ya maji safi na salama, kutokana na kuhofia endapo wakiendelea kuyatumia maji hayo huenda wakaathirika afya zao.

Licha ya tuhuma hiyo kuendelea kumtafuna Mwenyekiti huyo, pia analalamikiwa kwamba yeye pamoja na kamati yake ya maji wanadaiwa kula fedha za mchango ujenzi wa mradi wa maji shilingi milioni 21, ambazo zilichangwa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali.

Njafula ananyoshewa kidole kwa kutosoma mapato na matumizi ya kijiji kwa muda mrefu sasa na kutumia madaraka yake vibaya, kwa kuwagawia vipande vya ardhi baadhi ya marafiki zake kijijini humo bila kufuata taratibu.


Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa kikundi cha maji kijiji cha Matetereka, Fedrick Njarika alisema kuwa wanashindwa kusonga mbele kimaendeleo katika kuufanya mradi huo wa maji uwe endelevu kutokana na vikwazo vinavyojitokeza ambavyo vinasababishwa na Mwenyekiti huyo ambaye bado yupo madarakani.

Njarika alifafanua kuwa mradi huo wa maji baada ya kuchangishana fedha hizo wangeweza kuukamilisha ujenzi wake tokea mwaka 2012, lakini wameshindwa kufikia malengo husika kutokana na kero hiyo inayoendelea kurudisha nyuma ujenzi huo wa mradi wa maji wa kijiji hicho.

“Hata katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, Mbunge wetu Joseph Mhagama aliahidi kutuchangia kiasi cha shilingi milioni nane ili kuweza kufanikisha kukamilisha ujenzi wa mradi huu, ahadi ambayo ameitekeleza kwa kutoa milioni tisa lakini hadi sasa Mwenyekiti wa kijiji hiki hataki kutoa taarifa ya kupatikana kwa fedha hizi kwa wananchi wake”, alisema Njarika.

Aliongeza kuwa katika chanzo hicho ambacho kinategemewa kwa ajili ya kulisha maji wananchi wa kijiji cha Matetereka, hivi sasa kina hali mbaya kwani hata makopo na vizibo vya dawa hiyo ya kukaushia magugu yametupwa katika eneo la chanzo hicho.

Naye Benjamin Luambati ambaye ni Ofisa mtendaji wa kijiji hicho alisema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika waliofanya uhalifu huo, ili wananchi wasiweze kuathirika dhidi ya sumu ya dawa inayodaiwa kuwekwa kwenye maji hayo ambayo yalikuwa yakitumiwa na wakazi hao.

Vilevile Moses Njalika ambaye ni mkazi wa kijiji cha Matetereka alisema kuwa pamoja na ufuatiliaji kufanyika juu ya matumizi mabaya ya fedha hizo zilizochangwa na wananchi, hali inaonesha kuwa baadhi ya pesa wamekopeshana viongozi wa kijiji kinyume na taratibu ndiyo maana mradi huo unashindwa kukamilika ujenzi wake.

Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT kijijini hapo, Steven Mtema alieleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona watu walioweka sumu katika chanzo hicho wanaendelea kulindwa hivyo ni vyema serikali iwachukulie hatua za kisheria ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia mbaya kama hiyo.

“Binafsi naona kama hatupo salama, kwani nimeumizwa sana na vitendo vya ubabe na vitisho tunavyofanyiwa hapa kijijini kwetu mtu anavunja sheria kwa kulima kwenye vyanzo vya maji, huku akipuliza madawa ambayo ni sumu kwa binadamu na bado analindwa kwa maslahi ya Mwenyekiti baadhi tukihoji tunaonekana kuwa ni wakorofi”, alisema Mchungaji Mtema.

Alipotafutwa na mwandishi wetu ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo Mwenyekiti wa kijiji cha Matetereka, Njafula alionesha ukali na kugeuka kuwa mbogo huku akimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba haogopi kitu chochote na hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya wilaya au mkoa atakayeweza kumchukulia hatua dhidi yake.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema kwamba taarifa za matukio ya kijiji hicho Ofisi yake imezipata na kuahidi kwenda kufanya haraka mkutano na wananchi hao, ili kuweza kutatua kero hiyo mapema kabla madhara hayajatokea na kuathiri jamii.

“Hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria, watakaotuhumiwa wote na wale ambao wamelima kwenye vyanzo vya maji pale kijijini na kuweka hiyo sumu watachukuliwa hatua za kisheria”, alisisitiza Dkt. Mahenge.

No comments: