Sunday, October 23, 2016

MBINGA YAPIGA HATUA KATIKA KUPUNGUZA VIFO VYA AKINAMAMA WAJAWAZITO

Baadhi ya akinamama wajawazito wakiwa katika eneo la hospitali ya wilaya ya Mbinga.



Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepiga hatua katika kupunguza vifo vya akima mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka vifo 140 kati ya 100,000 kwa mwaka 2013 hadi kufikia vifo 40 mwaka 2015 hatua ambayo imeleta matumaini makubwa, kwa akina mama hao na jamii kwa ujumla wilayani humo.

Mafaniko hayo yametokana na mkakati kabambe wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ndani na nje ya wilaya hiyo ambao wamejiwekea, katika kuimarisha mfumo wa rufaa kwa akina mama wajawazito na kuwapatia elimu ya matunzo kwa wajawazito hao kuhusu umuhimu wa kuhudhuria Kliniki mapema na wakati wote wa ujauzito wao na mara baada ya kujifungua.

Pia elimu ya kujifungulia katika vituo vya afya na hospitali nao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo kwa akina mama hao pamoja na watoto wao, kwani pale wanapohitaji kutoka katika ngazi ya zahanati au kituo cha afya huchukuliwa kwa gari maalumu la kubebea wagonjwa bila malipo yoyote, tofauti na siku za nyuma walikuwa wakilazimika kuchangia kidogo.


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo ya afya na changamoto zinazoikabili hasa baada ya serikali kuigawa halmashauri hiyo na kuzaliwa kwa halmashauri nyingine ya mji wa Mbinga.

Samandito alifafanua kuwa kupungua kwa idadi ya vifo vya akina mama wajawazito ni faraja kubwa sio kwa wanawake wenyewe tu, bali hata kwa serikali ambayo imekuwa ikiboresha huduma mbalimbali za afya kwa wananchi wake kwa lengo la kuwa na kizazi chenye afya kitakachoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na mikakati iliyojiwekea halmashauri hiyo kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, ugawaji wa vyandarua, huduma ya dawa za ARV’s kwa akina mama wajawazito ambao wanamaambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, kuongezeka kwa vituo vya afya sambamba na kuboresha upatikanaji wa huduma ya damu salama katika vituo maalumu vilivyopendekezwa kutoa huduma hiyo.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa juhudi na nguvu ya pamoja kati ya halmashauri  na wananchi ambao kwa namna moja au nyingine, wamekuwa mstari wa mbele katika kujitolea na kuchangia shughuli mbalimbali katika maendeleo licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi za maisha yao ya kila siku.

Aidha aliongeza kuwa katika suala la kupungua kwa vifo vya akina mama wajawazito, lakini pia halmashauri hiyo imefanikiwa kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa hatari wa malaria ambao umekuwa ukiua watu wengi hapa nchini, kwani wilaya ya Mbinga imepunguza kutoka vifo 471 mwaka 2012 hadi kufikia vifo 42 mwaka 2014 na kwamba hivi sasa hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2015 idadi hiyo ilizidi kupungua hadi kufikia vifo 20 na hayo yametokana na dhamira ya dhati ya wilaya hiyo iliyojiwekea katika kupambana na magonjwa hayo.

Hata hivyo hata ugawaji wa vyandarua vyenye dawa umesaidia pia kupunguza ugonjwa huo katika wilaya ya Mbinga ambao ulikuwa ukiambatana na utoaji wa hati punguzo zaidi ya 20,015 ambazo zilizotolewa kwa akina mama wajawazito ambapo ni sawa na asilimia 89.5 huku vyandarua vilivyotolewa vimefikiaidadi ya 150,058 kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano na kwamba mwaka 2015 tayari ilishagawa vyandarua zaidi ya 250,169 kwa watoto wenye umri wa miaka mitano na kuendelea.

No comments: