Tuesday, October 4, 2016

RC RUVUMA ATOA WIKI MBILI KWA VIONGOZI MBINGA KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI MIHANGO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo katika kikao chake alichokifanya hivi karibuni wilayani Mbinga mkoani humo. 
Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

AGIZO limetolewa kwa viongozi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wahakikishe kwamba, wanasimamia kikamilifu na kumaliza haraka iwezekanavyo mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mihango kata ya Kigonsera wilayani humo na mwekezaji tarajiwa wa Kampuni ya AVIV Tanzania Limited.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge alitoa agizo hilo juzi alipokuwa katika kikao chake cha kazi na viongozi wa wilaya hiyo, kilichofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga iliyopo mjini hapa.

“Suala hili la mwekezaji natoa wiki mbili liwe limekamilika na taarifa kamilifu niipate haraka ofisini kwangu, nataka zingatieni kama taratibu za kutwaa eneo hili za wananchi zilifuatwa au la”, alisema Dkt. Mahenge.


Kadhalika Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa hataki kuona jambo hilo linalazimishwa au kukumbatiwa na viongozi wa serikali kwa kumbeba mwekezaji huku wananchi wakilalamika, badala yake amewataka wachukue maamuzi yenye busara ili kuweza kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza hapo baadaye.

Alisema kuwa anataka kuona mwananchi anatoa ardhi yake kwa kuridhika mwenyewe na sio kulazimishwa na kwamba wakati wa kutekeleza suala hilo ameagiza haki itendeke na ofisi yake, ipelekwe taarifa kamili juu ya idadi ya watu wangapi wanaokubali kutwaa ardhi yao na wale wasiokubali kupitia vikao husika vitakavyowashirikisha wananchi hao.

Mnamo mwaka 2014/2015 Kampuni ya AVIV Tanzania Limited ilitafuta eneo katika kijiji cha Mihango kata ya Kigonsera wilayani Mbinga, kwa lengo la kutaka kuzalisha zao la kahawa ambapo wananchi wengi wa kijiji hicho mpaka sasa hawataki kutoa ardhi yao kwa mwekezaji huyo kwa kile wanachoeleza kuwa watakosa eneo la kuzalisha mazao yao ya chakula na biashara na sehemu za kuishi, kutokana na wengi wao kuwa wahamiaji kutoka maeneo mengine ndani ya wilaya hiyo.


Wananchi wa kijiji hicho wanadai pia mwekezaji huyo hajafuata taratibu za utwaaji wa ardhi yao, hivyo hali hiyo ilisababisha kuleta mgogoro mkubwa uliodumu kwa muda mrefu kati ya uongozi wa wilaya, mwekezaji na wananchi hao hatua ambayo ilipelekea hata viongozi wa kata hiyo hivi karibuni kufanyiwa vurugu kwa kupigwa mawe na wananchi wa kijiji hicho wakati mwekezaji huyo alipoonekana akipita katika maeneo yao.

No comments: